NA RAYA HAMAD, OMKR

MAOFISA TEHAMA na wakuu wa vitengo wametakiwa kuwa wabunifu na kushirikiana katika majukumu yao ya kazi ili kuendana na kasi ya iliyopo ya ukuwaji wa teknologia ulimwenguni.

Mkurugenzi Mipango, sera na utafiti Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Daima Mohammed Mkalimoto alieleza hayo wakati akizindua mafunzo kwa maofisa tehama na wakuu wa vitengo wa ofisi hiyo na taasisi zilizochini yake kwenye ukumbi wa mkutano wa ofisi hio Migombani

Alisema serikali mtandao inatakiwa kuwa hai muda wote katika kutoa ushirikiano ili iwe ni suluhisho la kiutendaji katika mabadiliko na kufanya masuala ya tehama kuwa rahisi na kuwa na mfumo mmoja wenye tija kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Nae mkufunzi wa mafunzo hayo Ali Abdi Ali kutoka serikali Mtandao alisema maofisa TEHAMA ili waendane kasi ya mabadiliko ya mawasiliano ni muhimu wawe wanapatiwa mafunzo ya mara kwa mara jambo ambalo litapelekea kuwa umakini katika utendaji wao wa kazi.

Aidha washiriki wa mafunzo hayo waliishukuru Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na kuomba muendelezo wa mafunzo hayo ili kuwa weledi zaidi na kufahamu maendeleo ya mawasiliano ya TEHAMA.