NA HANIFA SALIM

MKUU wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Salama Mbarouk Khatib, amewataka maofisa utumishi kuhakikisha wanasimamia sheria na kanuni za utumishi wa umma ipasavyo ili kila mmoja aweze kutekeleza majukumu yake kama inavyotakiwa.

Alisema kuwa, baadhi ya watendaji katika taasisi na wizara mbali mbali hawafuati sheria za utumishi ipasavyo kama ambavyo sheria na kanunuzi za kiutumishi zinavyo elekeza.

Alieleza hayo alipokuwa akifungua mafunzo ya siku moja kwa maofisa utumishi wa taasisi mbali mbali kisiwani Pemba, katika ukumbi wa ofisi ya Rais Fedha na Mipango huko Gombani Chake chake yaliyoandaliwa na ofisi ya Rais katiba, sheria utumishi wa umma na utawala bora.

Alisema kuwa, maofisa utumishi wanawajibu mkubwa wa kuhakikisha wanasimamia kila mfanyakazi ili kila mmoja anatimiza wajibu wake sambamba na kuwapatia stahiki zao bila ya uonevu wa aina yoyote kwani baadhi yao wamekuwa waki toa stahiki kwa upendeleo.

“Tunazo taarifa kwa baadhi ya maofisa utumishi wamekuwa na tabia ya kuwapa pesa za likizo watendaji kutokana na urafiki walionao na wakamuacha mwengine ambaye alikwenda zamani hivyo si sawa na sio utendaji wa kazi unaotakiwa”, alisema.