NA ABOUD MAHMOUD

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Ofisi kuu ya Utumishi wa Umma imekamilisha zoezi la mapitio ya miundo ya taasisi kwa wizara zote.

Pia tayari imekamilisha zoezi la uandaaji wa miundo ya utumishi wa kada zote 220 iliyopo na imepangwa kuiwasilisha serikalini ili kupata ridhaa ya kusambazwa mawizarani na watumishi kupangwa kwa mujibu wa madaraja yao ya kazi.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Seif Shaaban Mwinyi wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo maofisa utumishi wa taasisi za umma uliofanyika katika ukumbi wa Shirika la Bima (ZIC) Mpirani mjini Unguja.

Alisema kwamba ofisi imerikodi jumla ya nafasi 491 za watumishi waliotoka kwenye utumishi wa umma kwa sababu mbali mbali kwa kipindi cha Januari hadi Julai mwaka 2021.

“Serikali inajiandaa kujaza nafasi hizi kwa njia ya ajira kwa kada ambazo haziwezi kuzibwa kwa njia ya uhamisho,” alisema.

Sambamba na hayo Katibu huyo alifahamisha kwamba Ofisi Kuu ya Utumishi wa Umma imekuwa ikichukua hatua kuhakikisha rasilimali watu iliyopo inapangwa vizuri, inaenziwa, inalindwa na kuendelezwa ili kazi ziendelee na huduma kupatikana kama kawaida.

Seif alieleza kwamba Ofisi ya Utumishi wa Umma inaendelea kutoa miongozo yenye lengo la kuendeleza utekelezaji wa masuala ya utumishi.

Alisema miongozo hiyo ni pamoja na taratibu za uhamisho, upimaji wa watumishi wa umma, upandishaji vyeo, mikataba ya wataka huduma, urithishaji uongozi, watumishi wa umma kushiriki katika siasa na mipango ya rasilimali watu.

Aidha Katibu Mkuu huyo alisema madhumuni ya kufanyika kwa mkutano huo ni kubadilishana mawazo juu ya mambo ya msingi katika utekelezaji wa masuala ya tasnia ya utumishi wa umma.