WASHINGTON, MAREKANI

MARAIS wa Marekani na Ufaransa wamekubaliana kuboresha uhusiano kati ya nchi zao kuendelea mbele.

Ufaransa ikikubali kwa upande wake imekubali kumrudisha balozi wake mjini Washington wakati White House ikisema ilifanya makosa kwa kuingia mkataba na Australia ambayo ilinunua teklonojia ya Marekani ya manowari za kijeshi badala ya ile ya Ufaransa, bila kushauriana na Paris.

Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya rais Joe Biden na rais Emmanuel Macron kuzungumza kwa njia ya simu, viongozi hao wawili walikubaliana kuanzisha mashauriano ya kina ili kujenga tena imani, na kukutana barani Ulaya mwishoni mwa mwezi Oktoba.

Walisema Washington iliahidi kuunga mkono operesheni za kupambana na ugaidi katika ukanda wa Sahel zinazoendeshwa na nchi za ulaya.

Mazungumzo ya simu ambayo yaliombwa na Washington, yalikuwa jaribio la kumaliza mvutano baada ya Ufaransa kuishtumu Marekani kwa kuisaliti Ufaransa, wakati Australia iliweka kando kandarasi ya dola billioni 40 kwa ununuzi wa manowari za kawaida za Ufaransa, na kuchagua manowari zinazotumia nyuklia kujengwa na teknolojia ya Marekani na Uingereza badala ya Ufaransa.

Ufaransa ilikasirika kutokana na makubaliano hayo ya ushirikiano wa kiusalama kati ya Marekani, Uingereza na Australia, na kuwaita nyumbani mabalozi wake kutoka Washington na Canberra.