LONDON, UINGEREZA
NCHI tatu washirika, Marekani, Uingereza na Australia zimeanzisha mkataba wa ulinzi katika ukanda wenye umuhimu kimkakati ulio kati ya Bahari ya Hindi na Bahari ya Pasifiki, ujulikanao kama Indo-Pasifiki.
Viongozi wa nchi hizo, Rais Joe Biden wa Marekani, Waziri Mkuu Boris Johnson wa Uingereza na Waziri Mkuu Scott Morrison wa Australia walizindua mkataba huo katika mazungumzo yao yaliyofanyika kwa njia ya video.
Chini ya ushirikiano huo, Australia itasaidiwa kupata teknolojia ya kuunda nyambizi yake yenyewe, itakayoendeshwa kutumia nishati ya nyuklia.
Hata hivyo, viongozi hao watatu wamesisitiza kuwa nyambizi hiyo haitobeba silaha za nyuklia.China imelaani ushirikiano huo ikiutaja kuwa ni wa kukurupuka, na kitisho kwa utangamano wa kikanda.