WASHINGTON, MAREKANI
UTAWALA wa Rais wa marekani Joe Biden umeanza kuwajuulisha magavana wa majimbo pamoja na waratibu wa wakimbizi kote nchini kuhusu idadi ya wakimbizi wanaotarajiwa kwa kila jimbo karibu 37,000 kutoka Afghanistan.
Jimbo la California linatarajiwa kupokea zaidi ya wakimbizi 5,200 kulingana na takwimu zilizotolewa na wizara ya mambo ya nje ya Marekani kuhusu program ya uhamiaji wa watu wa Afghanistan.
Majimbo mengine ni Alabama na Mississippi kulingana na maofisa wa wizara hiyo.
Hata hivyo majimbo ya Hawaii, South Dakota, West Virginia, Wyoming na Washington DC hayatarajiwi kupokea wakimbizi wowote kwenye kundi la kwanza lililotoroka Afghanistan wakati wa siku za mwisho za kuondoka kwa vikosi vya Marekani mwezi uliopita.
Utawala wa Biden uliliomba bunge kuidhinisha fedha zitakazo saidia kuwapa hifadhi wakimbizi 65,000 kutoka Afghanistan nchini Marekani kufikia mwisho wa mwezi huu, pamoja na wengine 95,000 kufikia September mwakani.
Biden alimteua gavana wa jimbo lake la Delaware Jack Markell kuongoza juhudi za kutoa hifadhi kwa wakimbizi kutoka Afghanistan hapa Marekani.