WASHINGTON, MAREKANI
MAREKANI, washirika na wabia wake wametangaza juhudi za pamoja ili kuhakikisha uhuru wa kutembea na kulindwa kwa haki za wanawake katika nchi ya Afghanistan inayodhibitiwa na Taliban.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken na mwenzake wa Ujerumani Heiko Maas walishirikiana kuandaa mkutano wa mtandaoni ulioijadili Afghanistan.
Mawaziri wa Mambo ya Nje na maofisa wengine kutoka nchi 22, Umoja wa Ulaya, Umoja wa Kujihami wa Nchi za Kaskazini mwa Atlantiki na Umoja wa Mataifa walishiriki.
Blinken na Maas baadaye walizungumza na wanahabari katika kambi ya jeshi la anga ya Marekani nchini Ujerumani.
Taliban iliwateua mawaziri wa serikali yake ya mpito, lakini Blinken alisema si jumuishi.Alisema orodha ya majina yaliyotangazwa inajumuisha hasa wanachama wa Taliban au washirika wao, na haina wanawake.
Maas pia alielezea wasiwasi akisema hawezi kuwa na mtazamo wa matumaini.China na Urusi zilizo na ushawishi kwa Afghanistan hazikushiriki mkutano huo.