Ataka wapewe mafunzo zaidi kuongeza uzalishaji

Abainisha mipango serikali namna itakavyo wawezesha 

NA RAJAB MKASABA

DHANA ya ujasiriamali ina maana pana sana ambapo miongoni mwa hizo ni kwamba, mjasiriamali ni mtu ambaye ana hamasa kubwa ya kuleta mabadiliko chanya katika hali yake ya kiuchumi ambaye ana tabia za kipekee ili kufanikisha azma yake hiyo kwa kujishughulisha (yaani kujiajiri) ili awe na hali nzuri zaidi kiuchumi.

Pia, katika hali nyingine mjasiriamali anaweza kuwa mtu yoyote ambaye anajishughulisha mwenyewe (amejiajiri) katika sekta fulani mfano kilimo, ufugaji au biashara.

Neno ujasiriamali lina asili ya kifaransa “Entreprendre” sawa na kutekeleza ama kufanya shughuli fulani mwenyewe katika uwanja wa kibaishara katika maana rahisi ni sawa na kuanzisha biashara ama shughuli ya kujiajiri.

Kwa mitizamo mbali mbali ya wasomi wanamuelezea mjasiriamali kama mtu anayeongoza, anayepanga na aliye na utayari juu ya hatari zozote zinazoweza kujitokeza katika biashara ama shughuli yake husika.

Mchumi Joseph Schumpeter kutoka nchini Austria, ameieleza dhana ya ujasiriamali kwa kuegemea mihimili ya ugunduzi ama ubunifu katika nyanja hizi mbili za kugundua ama kubuni.

Utajiri unapatikana pindi ugunduzi unapoenda sambamba na mahitaji, kwa mtazamo huu inaweza kusemwa kwamba kazi ya Mjasiriamali ni sawa na kuunganisha mbegu za vigezo fulani katika hali ya ugunduzi na ubunifu ili kutengeneza ubora na thamani kwa mteja kwa imani ya kwamba thamani itakayopatikana itafidia gharama za mbegu hizo na hatimae kutengeneza faida ya kutosha inayopelekea utajiri.

Watu wengi sana wamekuwa wakichanganya maana ya ujasiriamali na hatimae kupoteza maana halisi ya neno hilo la ujasiriamali kwani wengi hufahamu kuwa ujasiriamali ni kufanya biashara ndogo ndogo, wengine hudhani kufundishwa kutengeneza batiki, sabuni, mafuta ya kujipaka, achari ama visheti.

Hali hii huchangiwa sana na baadhi ya walimu ama wakufunzi ambao huipotosha jamii kwa kutangaza kuwa wanafundisha ujasiriamali halafu ukifika katika elimu zao huwa wanawafundisha watu namna ya kufuga kuku, kulima uyoga, kutengeneza batiki na vitu vyengine na kusahau kwamba ujasiriamali ni zaidi ya kutengeneza vitu au bidhaa.

Kama inavyotambulikana kwamba ujasiriamali ni jambo kubwa duniani kote na limebadilisha maisha ya watu wengi kutoka katika hali ya umasikini na kuwafanya wawe na kipato kikubwa. 

Kinachohitajika ni watu wawe mabunifu na majasiri wa kuzitumia fursa mbali mbali zilizomo katika jamii na mazingira inayoishi pamoja na kujifunza kutoka kwa wale waliofanikiwa.

Mafanikio makubwa yamepatikana katika nchi zilizowajengea mazingira mazuri wananchi wake walioamua kujiingiza katika shughuli za ujasiriamali.

Kadhalika dunia imeweka mifano  ya watu na taasisi zilizoanzishwa katika utaratibu wa ujasiriamali na hatimae kupiga hatua kubwa ya mafanikio ya kupigiwa mfano ambapo hata kwa upande wa Tanzania wapo wafanyabiashara wakubwa ambao chimbuko lao ni shughuli za ujasiriamali.

Semina wajasiriamali kizimkazi

Wale wote waliofanikiwa katika shughuli za ujasiriamali, wametafsiri kwa vitendo dhana ya ujasiriamali kwamba ni kuwa na ujasiri katika kutafuta mali, kwa njia za halali.

Kwa mujibu wa Joseph Schumpeter ambaye ni mwana uchumi aliwahi kusema kwamba “Ujasiriamali una maana ya utaratibu na uendeshaji wa shughuli za kibiashara kwa ubunifu kwa lengo la kupata faida na kuwa tayari katika kukabiliana na hasara yoyote itakayojitokeza”.

Kwa mnasaba wa maoni ya mtaalamu huyo wa uchumi, mjasiriamali lazima awe na mipango madhubuti ya uendeshaji wa shughuli yake ya kiuchumi, awe na ubunifu kwa azma ya kupata faida ya biashara yake ikiwa ndio lengo kuu la kufanya biashara kwa mfanyabiashara yeyote.

Hata hivyo, mjasiriamali hatakiwi aogope vikwazo ikiwa ni pamoja na kupata hasara hasa ikiaminika kwamba watu matajiri na maarufu duniani kote ikiwemo Zanzibar ni Wajasiriamali.

Vi vyema wajasiriamali wakajifunza kutokana na historia za watu matajiri kama vile “Bill Gates”, muanzilishi wa kampuni ya”Microsoft” kutoka Marekani, “Mark Zuckerberg”, ambaye ni mjasiriamali wa mitandao na mwanzilishi wa kampuni na mtandao wa “Facebook” na kwa upande wa hapa Zanzibar ni Said Salim Bakhressa mwanzilishi wa Kampuni ya “Azam Marine”.

Wajasiriamali wanaweza kujifunza mengi kutokana kwa wajasiriamali wenzao hao ikiwemo historia zao pamoja na maendeleo waliyoyapata kwa ujasiri na ubunifu wao katika shughuli za ujasiriamali.

Kwa kutambua umuhimu wa wajariamali Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi hivi karibuni katika ziara zake alizozifanya katika Mikoa na Wilaya zote za Unguja na Pemba alikukutana na makundi ya wajasiriamali mbali mbali.

Katika mikutano yake hiyo, Dk. Mwinyi aliwaeleza muelekeo na azma ya serikali ya awamu ya nane katika kuwaunga mkono wajasiriamali huku akitumia fursa hiyo kwa kutoa shukurani zake pamoja na kuwapongeza kwa kumuunga mkono na kumchagua kwa kumpa kura nyingi.

Akieleza hatua zitakazochukuliwa kwa ajili ya kuwasaidia wajasiriamali, Dk. Mwinyi katika ziara zake hizo alizitaja ni pamoja na kuwatafutia mitaji, soko pamoja na elimu itakayowasaidia katika kufanikisha shughuli zao za Ujasiriamali.

Hivi karibuni mnamo Agosti 23, 2021 Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi alizindua tamasha la Kizimkazi lililokwenda sambamba na semina ya uwezeshaji kwa wWajasiriamali kwa udhamini wa Benki ya CRDB.

Katika kuhakikisha kuwa wajasiriamali nao wananufaika kwa kuwepo kwa tamasha hilo, mama Mariam Mwinyi alilizindua tamasha hilo sambamba na semina hiyo kwa kutambua kwamba hiyo ni nafasi muhimu ya kuwajengea uwezo wajasiriamali kwa kuwaongezea maarifa na kutambua fursa mbali mbali wanazoweza kuzitumia ili shughuli zao wazifanye wka ufanisi na kuongeza tija.

“Malengo ya semina hii yanakwenda sambamba na dhamira ya werikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Dk. Hussein Ali Mwinyi ya kuwaletea maendeleo Wajasiriamali ili waweze kufanya kazi zao kwa tija na kuinua kipato chao”, alisema mama Mariam Mwinyi katika hotuba yake ya uzinduzi tamasha la Kizimkazi lililowashirikisha Wajasiriamali. 

Katika maelezo yake mama Mariam Mwinyi alisema kwamba serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuwasaidia wajasiriamali wakiwemo kinamama na vijana hatua ambayo itawasaidia kwa kiasi kikubwa katika kupambana na umasikini.

Aidha, aliongeza kuwa kwa lengo la kufanikisha shughuli za uwezeshaji, Serikali ya awamu ya nane imo mbioni kuunganisha shughuli za uwezeshaji ili kuongeza ufanisi katika kutoa huduma zake.

Alieleza kwamba hivi karibuni pia, Dk. Mwinyi amemteua Katibu Mkuu Maalum kushughulikia masuala ya Uwezeshaji katika Ofisi ya Rais Kazi na Uchumi na vile vile, Rais anaendelea kuzihamasisha taasisi za fedha zikiwemo Benki kuwapatia mikopo nafuu wajasiriamali.

Kwa hivyo, Mama Mariam Mwinyi alitumia fursa hiyo kuipongeza Benki ya CRDB kwa kuziunga mkono kwa vitendo juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane katika kuwasaidia na kuwajengea uwezo Wajasiriamali kwa mafunzo kupitia Tamasha hilo la Kizimkazi.

Semina wajasiriamali kizimkazi

Tamasha hilo limekuwa na mchango mkubwa katika kuchochea shughuli mbali mbali za kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kuondokana na changamoto za kijamii hasa kwa Wajasiriamali.

Aidha, mama Mariam Mwinyi alitumia fursa hiyo kumpongeza mlezi wa tamasha hilo la Kizimkazi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha kuwa Tamasha hilo linaendelea na linafanikiwa kila mwaka.

Tangu kuanzishwa kwa Tamasha hilo CRDB imekuwa ikiwawezesha wananchi wakiwemo wajasiriamali kwa kuwapa mitaji ili waweze kusonga mbele kiuchumi ambapo ilitenga kiasi cha shilingi milioni 20 kwa zawadi mbali mbali kwa ajili ya washindi walioshiriki katika michezo mbali mbali katika Tamasha la mwaka huu.

Sambamba na kutenga kiasi cha shilingi milioni 500 kwa ajili ya uwekezaji kwa wananchi wa vijiji vinavyoandaa tamasha hilo vikiwemo Kizimkazi Mkunguni, Kizimkazi Dimbani na Kibuteni, pamoja na kuweka ahadi ya kutoa mkopo kwa ajili ya ujenzi wa soko pamoja na kituo cha gari katika eneo hilo la Kizimkazi.

Tamasha hilo la siku sita la Kizimkazi ambalo liliwashirikisha wajasiriamali, lilianza mnamo Agosti 23,2021 ambalo lilizinduliwa na mama Mariam Mwinyi na kufungwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan ambalo liliadhimishwa kwa shughuli mbali mbali zikiwemo elimu, utamaduni, sanaa, michezo pamoja na utoaji wa chanjo ya UVIKO 19.