NA MARYAM SALUM, PEMBA
ULE wakati wa zama ya mwanamke hawezi kuwa kiongozi kwa wakati huu hazina nafasi tena na kwamba wanawake wako bega kwa began a wanaume kwenye mambo mbalimbali alimradi hayaendi kinyume na mila, silka, utamaduni hata dini.
Na ndio maana leo hii hapa Zanzibar wanawake ni wataalamu wa fani mbalimbali kama udaktari, mainjinia na kazi mbalimbali ambapo hapo kabla hawakuzifanya.
Kwa upande wa uongozi wanawake wengi wamshika nyadhifa za juu serikalini jambo ambalo linaonesha dhahiri kuwa wanaweza kwa kuwa wengi wao wanapopewa nafasi hufanya vyema kuliko wanaume.
Katika makala haya tutamzungumzia mmoja wa mwanasiasa ambae ni mbunge wa viti maalumu katika mkoa wa Kusini Pemba.
Maryam Azan Mwinyi, alizaliwa mwaka 1972 mjini Unguja na amebahatika kusoma hadi kidato cha nne na kubahatika kupata elimu ya juu ya shahada ya kwanza ya rasilimali watu na uongozi.
Mbunge huyo akitoa historia yake ndogo ya kisiasa alisema, yeye ni mwanachama wa Chama cha Mapinduzi CCM tsngu mwaka 1995, na hadi leo hii bado anaendelea kukitumikia Chama na Wananchi kwa ujumla.
Alisema katika chama aliwahi kushika nafasi ndogo ndogo za uongozi ikiwemo mjumbe wa maskani tawi la Tibirinzi, Katibu wa UWT wa tawi hilo, Katibu mkuu Jimbo mwaka 2018 na baada ya hapo kuwa Mjumbe Mkutano mkuu Jimbo hadi amekuwa Mbunge.
Alisema miaka ya nyuma baadhi ya maeneo hapa visiwani kulikuwa na mtazamo mbaya kwa jamii, jambo ambalo lilipelekea wanawake kuendelea kubaki nyuma katika nafasi za uongozi na kimendeleo kwa ujumla.
“Naweza kusema kwamba kilichowafanya wanawake hapo zamani kutokuwa na mashirikiano kwa wanawake wenzao wanapojitokeza kugombea ni kutokana na kukosa uelewa juu ya umuhimu wa kuwachagua wanawake kwenye nafasi za Uongozi,” alisema Maryam Azan.
Alieleza kutokana na kukosekana kwa uelewa huo kwa wananchi hasa kwa wanawake ilipelekea kuwepo kwa mfumo dume ambao uliathiri jamii na hadi leo bado wapo baadhi yao wanauendeleza.
“Kabla hatujapatiwa uelewa elimu inayohusiana na umuhimu wa wanawake kujitokeza katika kugombea nafasi mbali mbali za uongozi, na kuwachaguwa katika nafasi hizo, jambo hili lilisababisha akina mama wengi kukosa haki zao za msingi,” alisema Mbunge huyo.
Maryam, alieleza kutokana na woga waliokuwa nao akinamama katika kujitokeza kugombea nafasi za uongozi hapo zamani iliwafanya kukosa fursa hizo na kuwaachia wanaume pekee yao, jambo ambalo limeifanya jamii ya kiume kuendeleza mtazamo wao huo na kuona kwamba mwanamke si mtu wa kuongoza.
“Kama mwanamke hapo zamani walikuwa wakiogopa kutokana na familia kuonekana kwamba mwanamke si mtu wa kujitokeza mbele mbele kwenye nafasi kama hizo za uongozi, ni kutokana na mwamko mdogo kwa wanawake kugombea hizo nafasi,” alisema.
Akizungumzia suala la changamoto katika kugombea nafasi za uongozi kwa wanawake, alisema ni suala la kawaida kwani kwenye jamii hakuna mema matupu, kunakuwepo na watu tofauti wenye mitazamo tofauti, watu wote hawapo sawa hususani kumuona mwanamke kujiingiza kwenye suala la maendeleo.
Akielezea jinsi yeye alivyopata mashirikiano wakati wa kugombea nafasi hiyo, alisema kwamba wapo waliosema maneno mengi yenye lengo la kumkatisha tamaa kwa nia ya kumfanya avunjike moyo na kutofikia yale malengo aliyoyakusudia katika ndoto zake za maisha.
“Mimi binafsi wapo watu nawajua wakaribu walisema mengi, na kama sikuwa mwanamke mwenye kujiamini na mwenye subra basi kwakweli nisingalifika hapa nilipofika kwani yanakatisha tamaa kutofikia ndoto za maisha,” alieleza.
Alisema ni haohao wanawake wenziwe ndio walioonesha dharau na kebehi jambo ambalo lilionesha dhahiri kuwa wana choyo na roho mbaya.
Alieleza kuwa mtu akitaka kugombea nafasi za uongozi lazima kwanza ajenge uaminifu kwamba litakalo tokea lolote atapambana nalo bila woga ili makusudi kufikia ndoto zake, kwani wajumbe husema mengi yakukatisha tamaa.
Alisema licha ya changamoto alizokumbana nazo kwa baadhi ya wajumbe, lakini walikuwepo baadhi yao walimpa mashirikiano yakutosha na kufika hapo alipofika.
“Mimi kama sina moyo wa subra kwa maneno ambayo nilikuwa napakaziwa, basi ningalikuwa kila siku nagombana na watu,hivyo subra na uaminifu ndio sialaha yangu iliyonisaidia kufikia hapa,” alieleza.
Alifahamisha kuwa kitu kilichomshawishi kuingia kwenye uongozi ni kutokana na kuwasaidia wanawake wenzake na wananchi kwa ujumla kwa kutaka kutekeleza yale aliyoahidi wakati akiomba kura.
“Mimi nilipoingia katika hii nafasi sikuingia tu kwa maslahi yangu binafsi, kujifurahisha, au tamaa ya kitu bali niliingia kujenga chama, wananchi na wanawake, kwa malengo niliokwisha yaeleza,” alisema.
Alivitaja vikwazo vyengine kuwa ni pamoja na watu kumzushia mambo yasiyo na maana ikiwa ni pamoja na kwamba akipata atakuwa na dharau, kutoileta maendeleo, kuwa na tamaa n ahata jeuri, jambo ambalo alisema kuwa hayo yote hayana nafasi kwake.
“Lakini propaganda zao ama hisia zao zilivyo lenga sivyo, na sasa zimekuwa ni tofauti kwani wao wenyewe wameanza kuona mengi ninayoyafanya kwa wananchi kwa kipindi kichache toka nipate nafasi hii,” alieleza.
Alieleza kuwa tangu kuanza kuitumikia nafasi hio ameshafanya mambo mengi ikiwa ni pamoja na kutenga muda wa kuzungumza na wananchi, kusikiliza matatizo yao sambamba na kuyapatia ufumbuzi kwa yale anayoyaweza.
Mbunge huyo aliyataja mambo aliyoyatekeleza kuwa ni pamoja na kutoa elimu juu ya ujasiriamali kwa wajasiriamali wa Mkoa huo elimu yenye lengo la kuwafanya kubuni bishaa na kuzitengeneza ili kuona wanajitegemea kimaisha.
Kuhusiana na familia yake, alisema ilimpa ushirikiano wa kutosha jambo ambalo lilimfikisha hapo alipo.
“Katika suala la mashirikiano kwenye familia yangu akiwemo mume wangu tangu nianze hadi sasa kwa kweli anaonesha yuko pamoja na mimi, jambo ambalo nimefikia malengo”, alisema.
Aliisihi jamii wakiwemo wanawake na wanaume kuwachagua wanawake wanapojitokeza katika nafasi za uongozi na kuondosha mfumo dume ulioota mizizi baadhi ya jamii.
Hata hivyo alitoa wito kwa viongozi wenzake wanawake kutekeleza ahadi walizoziweka kwa jamii wakati walipoomba kura ikiwemo kusikiliza kero zao ili kujenga matumaini kutoka kwao.