LONDON, England
KOCHA wa kituo cha kukuza na kuendeleza vijana cha klabu ya Arsenal, Per Mertesacker, amewaambia mashabiki timu hiyo watarajie kuingia kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya miaka mitatu ijayo.

Arsenal wameanza ligi msimu huu taratibu na inaonekana kuwa wanaweza wakashindwa tena kupata nafasi ya kucheza michuano hiyo mikubwa Ulaya.
Mertesacker, amesema, pamoja na mwanzo huo bado mashabiki wa Arsenal wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanamuamini kocha wao, Mikel Arteta, kwani huko mbele anaweza kufanya vizuri.

Kocha huyo raia wa Ujerumani ambaye aliwahi kuwa beki wa zamani wa Arsenal, alisema, ni mapema kwa sasa kujadili kuhusu mustakabali wa msimu huu.”Nafikiri kila mmoja anafahamu kuwa baada ya kocha Arsene Wenger kuondoka Arsenal, ilikuwa inatakiwa ipite miaka kadhaa ili gepu lake lizibwe.”

“Nafikiri kwa sasa mashabiki wa Arsenal wanatakiwa kusubiri misimu mitatu au minne ili kupata nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.””Nafikiri kocha Mikel anatakiwa kupewa muda ambao anautaka na baadaye ataleta matunda bora kwenye klabu, sidhani kama ni sahihi sasa kufikiri kuhusu njia ya mkato.””Hata mimi nataka kuona Arsenal inaingia Ulaya hata kesho, lakini, naamini kila kitu kinahitahji muda wa kutosha”, alisema, beki huyo.

Arsenal imeanza msimu huu vibaya ambapo kwenye michezo mitano ya ligi imeshapoteza mitatu dhidi ya Brentford, Chelsea na Manchester City huku ikishinda dhidi ya Norwich City na Burnley. (Goal).