NA HAFSA GOLO
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Sera, Uratibu na Shughuli za Baraza la Wawakilishi, Dk. Khalid Salum Mohamed, amewataka masheha kufichua mambo yanayosababisha uvunjifu wa sheria za nchi na kufanyika makosa ya jinai.
Aliyasema hayo wakati akizindua zoezi la utoaji elimu kwa masheha katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul Wakili Kikwajuni Mjini Unguja.
Alisema hatua hiyo itasaidia kwa serikali kuwatambua wafanyaji biashara za dawa za kulevya, udhalilishaji, wizi pamoja na wageni wanaoingia kinyume na taratibu za nchi.
Aliwataka masheha hao kuzingatia mambo ya msingi katika kusimamia majukumu yao ya kazi, ikiwemo uongozi bora, mfumo wa uendeshaji, udhibiti na nidhamu katika uwajibikaji wa majukumu yao.
Alifahamisha kuwa endapo watafuata misingi hiyo wataepuka kujihusisha na migogoro ya ardhi, vitendo vya rushwa, kushirikiana na wahalifu katika kufanya makosa.
Dk. Khalid, alitumia fursa hiyo kupongeza juhudi za Idara ya Uhamiaji Zanzibar, kwa kuandaa zoezi hilo muhimu la kuwajengea uwezo masheha na kubadilishana uzoefu katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi na wageni wanaofika katika ofisi mbali mbali za Uhamiaji.
Hivyo alisisitiza kuwa suala la usalama wa nchi na uendeshaji mzuri wa shughuli za serikali kutambua kwamba masheha ndio viongozi wa awali wanaosimamia mambo hayo kwa kuhakikisha mazingira na nyenendo ya watu inakuwa katika utaratibu unaokubalika.
Sambamba na hilo, alisema suala la uhamiaji ni muhimu na haliepukiki katika kuimarisha maendeleo ya uchumi wa taifa lolote duniani, hivyo ni wajibu kuhakikisha wageni wote wanaoingia nchini wanafuata taratibu na sheria za nchi.
Alihimiza pamoja na mchango huo mkubwa unaotolewa na wageni hao ni lazima kuhakikisha wanafuata sheria na maadili ya nchi, kwani kuna baadhi ya wageni wasio waaminifu wanaweza kuingia na kuhatarisha usalama wa nchi.