MWANAJUMA ABDI, DAR ES SALAAM

RAIS wa Kampuni ya Rena Events Ltd ya Tanzania Rena Callist amesema mashindano ya ‘Miss East Afrika’,  yatafanyika Novemba 26  mwaka huu.

Mashindano hayo yatashirikisha nchi 16, ambayo yatakuwa na lengo la kutangaza vivutio vya utalii, utamaduni,fursa za uwekezaji na biashara nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari, jana amesema mashindano hayo yatawashirikisha  walimbwende kutoka nchi 16 za Afrika Mashariki  kuanzia umri wa miaka 18 – 26, ambapo washiriki lazima watoke katika nchi husika ( raia).

Alisema mbali ya kuwa ya ulimbwende pia yamejikita katika kutangaza vivutio vya utalii, utamaduni, uwekezaji na biashara kwa Tanzania kwa vile yatarushwa moja wa moja na vyombo vya habari ikiwemo na mitandao ya kijamii, ambapo  zaidi ya watazamaji milioni 300 wataangalia katika pembe zote za dunia.

Alieleza washiriki wa mashindano hayo wataomba kwa njia ya mitandao‘website’, halafu watafanyiwa mchujo na kupatikana washiriki 16 kwa nchi 16 zitazoshiriki ikiwa Tanzania ndio mwenyeji wa mashindano hayo.

Alivitaja vigezo vya ushiriki wa mashindano hayo ni kuwa raia wa nchi husika, elimu ya sekondari na kuendelea, tabia mzuri katika jamii na kuelezea nchi yako kwa ufasaha.

Alizitaja nchi zitazoshiriki ni pamoja na Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, Ethiopia, Eritrea, Djibouti, Somalia, Malawi, Seychelles, Comoro, Madagascar, na Mauritius, ambapo mshindi wa kwanza atapata zawadi ya gari la kisasa aina ya Nissan X Trail yenye thamani ya shilingi milioni 110.

Alisema mshindi wa pili atapata shilingi milioni 11, na mshindi wa tatu atapata shilingi milioni 5, pamoja na zawadi mbali mbali zenye thamani ya shilingi milioni 20, ambapo zawadi zote zinathamani ya shilingi milioni 146.

Naye Kaimu Katibu Mtendaji wa BASATA, Matiko Mniko alisema serikali inaipongeza kampuni hiyo, kwa kuyarejesha mashindano , ambayo itaitangaza Tanzania kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Mapema Makamu wa Rais wa Kampuni ya Rena Events Ltd Tz, Jolly Mutesi alisema mashindano hayo yatatoa fursa ya kuwanyanyua wanawake katika ajira na kuwaongezea kipato.