NA MWAJUMA JUMA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ, Masoud Ali Mohammed, amesema udhalilishaji wa kijinsia ni janga ambalo kuondoka kwake ni kuachana na muhali.

Masoud aliyewakilishwa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharib, Rashid Khadid Rashid, aliyasema hayo katika mafunzo ya siku moja juu ya kuzuia ukatili wa kijinsia kwa watoto, usalama barabarani, zimamoto na uokozi na athari za dawa za kulevya yaliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh  Idrissa Abdulwakil Kikwajuni mjini Unguja.

Alisema Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amelivalia njuga janga hilo kwa kuanzisha mahakama maalumu ya udhalilishaji lakini licha ya juhudi hizo bado inaonekana kuongezeka kutokana na jamii kutokubaliana na suala zima la kuacha muhali kwa watuhumiwa.

“Ukiangalia wengi ambao wanafanyiwa vitendo hivyo ni watoto wadogo, na wafanyaji ni ndugu wa karibu, waalimu wa madrasa na skuli, kwa kweli inasikitisha kujua wanafanya hivi kwa sababu gani”, alisema.

Hivyo aliwataka viongozi wa shehiya kuendelea kuziimarisha kamati zao kupambana na vitendo vya udhalilishaji, pamoja na kuihamasisha jamii kuachana na muhali juu ya wale wanaopatikana na makosa hayo.

“Tuwafikirieni watoto wetu wadogo, tukifanya mchezo tutakosa maimamu na viongozi na hili lifanywe kwa kushirikisha jamii”, alisema.

Kuhusu dawa za kulevya alisema sio kweli kama watoto wao wanajihusisha na utumiaji wa dawa hizo kwa kukosa ajira bali ni mmong’onyoko wa maalidi na dini kutokufuatwa ipasavyo.

Rashid ambae pia ni Mkuu wa mkoa Kusini Unguja, akizungumzia kuhusu suala zima la usalama barabarani alisema katika mkoa wake wa Kusini tokea Novemba hadi Julai mwaka huu, ajali 37 za barabarani zimetokea na watu vijana 32 walifariki, ambazo zimechangiwa na utumiaji wa dawa za kulevya.