NA AMEIR KHALID, PEMBA
MKUU wa Mkoa wa Kusini Pemba Matar Zahor Masoud amesema wazanzibari, wana kila sababu ya kuheshimu mawazo na fikra za mzee Karume kutoka na mambo mengi ya msingi aliyoyafanya.
Alisema mzee Karume alikuwa kiongozi wa kuigwa kutokana na mambo mengi aliyoyafanya, ambayo hivi sasa bado ni faida kwa Zanzibar.
Mkuu huyo wa mkoa alitoa kauli hiyo huko viwanja vya michezo Chuo cha Amali Vitogoji Pemba, mara baada kuongoza maandamano ya wanamichezo na walimu mbali mbali, ikiwa ni ufunguzi wa tamasha la miaka 57 ya elimu bila malipo jana asubuhi.
Alisema kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar suala la kupata elimu kwa wazanzibari lilikuwa jambo gumu, lakini baada ya mapinduzi mzee Karume kwa kutumia busara zake aliamua kutangaza suala la elimu kuwa ni bila malipo.
‘’Kabla Mapinduzi skuli zilikuwa chache sana na wananchi wengi maskini walishindwa kupata elimu, lakini juhudi za mzee Karume kutanga elimu buila hivi sasa kila mmoja anaona juhudi hizo na wananchi wanapata elimu bila matatizo’’alisema.
Matar alisema serikali ya Zanzibar ina nia nzuri ya kutoa elimu kwa kila mwanachi na miundo mbinu mizuri inawekwa, ili elimu hiyo ipatikane bila kuzuzizi,hivyo ni vyema wanafunzi kutumia fursa hiyo kutafuta elimu ili iweze kuwasaidia katika maisha yao.
‘’Wanafunzi tambueni fika kuwa elimu ni kitu pekee ambacho kitaleta maendeleo ya Zanzibar, hivyo msichoke kutafuta elimu ili kuijenga Zanzibar yenu’’alisisitiza.