WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amemtaka mkandarasi Power Construction Cooperation Ltd kutoka China anayejenga Daraja jipya la Wami kuongeza kasi ili kukamilisha ujenzi kabla ya muda walioongezewa kwenye mkataba kumalizika.

Prof. Mbarawa aliitoa agizo hilo wakati akikagua maendeleo ya daraja hilo  lenye urefu wa mita 510, upana wa mita 11.85 lililoko mkoani Pwani.

Daraja hilo ni kiungo muhimu kutoka Mji wa Chalinze kwenda mikoa ya kaskazini mwa nchi  na nchi za jirani.

Akiwa katika ukaguzi huo, profesa Mbarawa alisema ujenzi wa mradi huo kwa sasa umefikia asilimia 61, ulitarajiwa kukamikika Septemba mwaka huu.

Alisema  ila kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza ikiwemo mvua kubwa zilizonyesha mwaka jana pamoja na ucheleweshaji wa vifaa kuingia nchini kulikosababishwa na mlipuko wa  uviko -19, Mkandarasi aliongezewa  muda hadi Novemba, 2022.

“Hakikisheni mnajipanga vizuri pamoja na kuongeza saa za kufanya  kazi hata nyakati za usiku ili kukamilisha ujenzi kabla ya muda ulioongezwa” alisema Prof. Mbarawa.

Aidha, Waziri Mbarawa alimhakikishia mkandarasi huyo kuwa Serikali itaendelea kutoa fedha kwa wakati na kumtaka kuhakikisha anaongeza kasi ya ujenzi kwa kuzingatia viwango vilivyoweka ili daraja hilo liweze kudumu.

Awali akitoa taarifa ya mradi huo kwa Waziri Mbarawa, Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mhandisi Andrew Kasamwa, alisema gharama ya mradi wa ujenzi huo  ni Sh. bilioni 72 ikiwa ni fedha za malipo ya mkandarasi  na mhandisi – mshauri.

Mhandisi Kasamwa alisema kuwa kwa sasa kasi ya ujenzi inaendelea vizuri na tayari nguzo za daraja zimekamilika kwa asilimia 100, ujenzi wa kuta mbili za mwanzo na mwisho wa daraja umekamilika kwa asilimia 85.