NA ASYA HASSAN

MBUNGE wa Jimbo la Tunguu Wilaya ya Kati Unguja, Khalifa Salim Suleiman, amesema utengenezaji wa barabara tano za ndani zenye urefu wa zaidi ya kilomita nane katika jimbo la Tunguu utakamilika ndani ya miezi miwili ijayo.

Khalifa alisema hayo wakati wa ziara ya ukaguzi wa barabara hizo pamoja na ujenzi wa tawi jipya la CCM Kikungwi ikiwa ni kuangalia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi.

Alisema sehemu nyingi katika jimbo hilo zimekuwa na changamoto ya barabara za ndani hazipitiki hasa kwenye kipindi cha mvua hivyo kukamilika kwa matengenezo hayo kwa hatua ya kifusi kutasaidia wananchi kuondokana na changamoto hiyo.

Mbali na hayo Mbunge huyo alilazimika kuanzisha njia mbadala itakayotumika badala ya ile ya zamani ambayo imekatiza katikati ya skuli ya Kibele kwani imekuwa kero kwa walimu na wanafunzi zikiwemo ajali za mara kwa mara, vitendo vya udhalilishaji pamoja na wanafunzi kutokupata kusoma kwa utulivu.

Kwa upande wake Katibu wa CCM, mkoa wa Kusini Unguja, Suleiman Mzee Suleiman ‘Charas’, alisema ziara hiyo ililenga kukagua miradi ya wananchi inayotekelezwa na viongozi wa majimbo wakiwemo wabunge na wawakilishi ili chama kiweze kujiridhisha juu ya utekelezaji wa ilani ya chama hicho katika miradi hiyo.

Nae Mwalimu Mkuu Msaidizi wa skuli ya sekondari Kibele, Mohammed Ali Miraji na Katibu wa Kamati ya ujenzi wa barabara hizo, Ali Mussa Ali walisema wamefurahishwa na ujenzi wa njia hizo kwani zitasaidia kuondosha changamoto zilizokuwa zikiwakabili.

Katika utekelezaji wa mpango huo, wananchi wa wadi ya Bungi na Tunguu  watanufaika na ujenzi wa barabara hizo ambazo zitagharimu zaidi ya shilingi milioni 500 za kitanzania.