WAJERUMANI wanapiga kura katika uchaguzi ambao utakamilisha muhula wa mwisho wa Angela Merkel kama kansela wa Ujerumani na kumuweka kiongozi mpya atakayekuwa muendeshaji mkuu wa taifa hilo liliopo barani Ulaya.

Merkel anaondoka madarakani baada ya kushikilia usukani wa kuliongoza taifa hilo kama mkuu wa shughuli za serikali kwa muda wa miaka 16, lakini suali liliopo ni je historia itamkumbuka vipi je?

Katika kipindi cha miaka 16 ya uongozi wake, Merkel amebadilisha siasa za Ujerumani na kuendelea kuliweka taifa hilo kwenye medani za juu za kisiasa duniani kutoka kanda ya Ulaya.

Kabla ya Merkel kuchukua nafasi ya kuiongoza Ujerumani siasa za nchi hiyo kwa kiasi kikubwa zilitawaliwa na wanaume yaani kama klabu cha wanaume, lakini chini ya uongozi wake mambo yamekwenda kisera zaidi.

Mhadhiri wa siasa za Ujerumani na Ulaya katika chuo kikuu cha Birmingham nchini Uingereza, Charlotte Galpin alisema kuwa Merkel amekuwa akitajwa katika jarida la Forbes kuwa mwanamke mwenye nguvu sana duniani tena kwa miaka 10 mfululizo.

Nafasi yake imekuwa ikiwakilisha umuhimu wa nafasi ya mwanamke na anajulikana kwa kuwaweka wanawake katika nafasi muhimu za maamuzi katika serikali yake.

Merkel alichukua uamuzi kumuunga mkono mwanasiasa mwanamke kutoka nchini Ujerumani, Ursula von der Leyen, kuwa waziri wa kwanza wa ulinzi mwanamke nchini Ujerumani ambapo hivi sasa mama huyo ndiye rais wa Tume ya Ulaya.

Naye Prof. Rüdiger Schmitt-Beck mtaalamu wa sayansi na siasa ya kijamii katika chuo kikuu cha Mannheim, alisema sera zake ndio urithi atakaouacha ambao umechanganyika na siasa za kushangaza.

Masuala mengi ya kisasa kama ndoa ya jinsia moja, nishati ya nyuklia, na kukaribisha sera za uhamiaji zisingetarajiwa kutoka kabisa kwa kansela wa chama cha Christian Democrats.

Wakati Angela Merkel anajiandaa kuondoka madarakani huku mazingira ya kisiasa yakiwa si mazuri, hali hiyo inaleta hofu kwa kiasi fulani kuwa mfumo wa chama unazidi kuwa mgumu na chama cha AfD ambacho, kinapinga sera ya uhamiaji.

Hata hivyo, ukweli ni kuwa alikuwa kansela wa kwanza mwanamke ambaye mtindo wake wa kuongoza ulizingatia sana busara hali ambayo itakuwa nafasi nzuri ya kuiga kwa atakayekuwa mrithi wake atakayechaguliwa.

Naye, Dk. Katrin Schreiter, ambaye ni mhadhiri wa masomo ya kijerumani na Ulaya katika chuo cha Kings kilichopo mjini London, alisema Merkel anaondoka madarakani akiwa bado kuna mambo hakuyamaliza kuyatekeleza.

Pamoja na kwamba oongozi wake ulikuwa unakosolewa vikali na baadhi ya makundi ya watu nchini Ujerumani kwa kukosa maono, hata hivyo cha kushangaza ni kwamba watu waliendelea kumpigia kura.

Jambo jengine la kukumbukwa analoliacha ni kwamba aliiweka ajenda ya chama chake cha Christian Democrats kwa kusogeza wahafidhina karibu na wale wa mrengo wa kushoto wa Greens ambao ndio walikuwa wakosoaji wakubwa wa serikali yake.

Hata hivyo, Matt Qvortrup alisema anaamini kuwa Merkel alikuwa ni nguzo kubwa ya kunusuru uchumi hasa kwenye kipindi ambacho bara la Ulaya lilipitia kwenye mdodoro wa mnamo mwaka 2008.

Sarafu ya Euro, ambayo ni moja ya viashiria imara zaidi vya muungano wa Ulaya, ilikabiliwa na shinikizo la mdororo wa uchumi, na kupelekea moja ya kauli maarufu za Merkel alipoonya kwamba “Euro ikifeli, basi Ulaya inafeli.”

Chini ya Merkel, taifa lake lenye uchumi imara zaidi katika kanda ya Umoja wa Ulaya lilijitwika jukumu la uongozi barani Ulaya.

Kwa upande mmoja, serikali ya Ujerumani ililaazimisha hatua kali za kubana matumizi na mageuzi hasa kwa mataifa yenye mzigo mkubwa wa madeni nchini Ugiriki, baadhi ya wakosoaji walitoa hata ulinganisho na ukaliaji wa Ujerumani wakati wa vita vikuu ya pili vya dunia.

Kwa upande mwingine, Merkel aliidhinisha msaada mkubwa kwa mataifa ya Ulaya. Dhamana ya Ujerumani kwa madeni ya mataifa mengine iliongezeka pakubwa.

Ukweli kwamba sehemu iliyobaki ya Umoja wa Ulaya, kwa ujumla ulikubali jukumu jipya la uongozi wa Ujerumani pia ulitokana na haiba ya Merkel.

Kuna muda wakimbizi kutoka mashariki ya kati walikuwa wanafika Ulaya, Markel hakusita kufungua mipaka kwa mamilioni ya wakimbizi kuingia nchini Ujerumani alikuwa na kauli yake maarufu ya “wir schaffen das” – tunaweza kudhibiti hili.

Jambo jengine ambalo alilisimamia kansela Merkel ni kuhusu tukio la waziri wa fedha walipohutubia taifa mwaka 2008 waliwahakikishia wananchi wake kuwa wataimarisha uchumi hasa kwenye kipindi ambacho kilikuwa kigumu kwa serikali ya Ujerumani.

Katika miaka yake 16 kama kansela, Angela Merkel ameweka alama kwenye sera ya kigeni ya Ujerumani, ambapo jukumu la taifa hilo katika ulimwengu limeongezeka sana, kama ilivyokuwa kwenye changamoto za kisiasa za uliwengu.

Ni wachache sana nje ya Ujerumani waliomfahamu Angela Merkel wakati alipochaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa kansela mwaka 2005 na ni wachache pia walifikiria ni kwa kiwango gani angeshawishi siasa za ulimwengu.

Alianza haraka kujiamini, kote nyumbani na nje. Kuanzia mwanzo, aliunda kwa sehemu kubwa mkakati wa sera ya kigeni wa serikali yake mwenyewe, kuliko kumuachia jukumu hilo waziri wa mambo ya kigeni.

Kama mwenyeji wa mkutano wa kilele wa viongozi wa mataifa manane yalioendelea kiviwanda G8, uliofanyika katika eneo la mapumziko la pwani ya Baltic la Heiligendamm mwaka 2007, alikuwa tayari anashughulikia kwa kujiamini, wakuu muhimu zaidi wa mataifa na serikali duniani.

Kansela Merkel aliendeleza sera ya kigeni ya serikali zilizotangulia, ya kutoegemea upande, inayozingatia biashara, na kukubaliana na pande zote pale inapowezekana wakati ikiwa na jicho kwenye maslahi ya kiuchumi ya Ujerumani kote duniani.