NA MWANDISHI WETU
KIWANGO cha mfumko wa bei wa mwaka ulioishia Agosti 2021 umepungua kidogo hadi asilimia 2.1 kulinganisha na asilimia 2.2 kwa mwaka ulioishia Julai 2021.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Kitengo cha Takwimu za Bei Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Khamis Abrahman Mshamu, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari huko Mazizini mjini Unguja.
Alisema, kiwango cha mfumko wa bei za vyakula na vinywaji visivyo na vileo kilipungua hadi asilimia 0.4 hasi mnamo Agosti 2021 kutoka asilimia 1.2 iliyorekodiwa mnamo Julai 2021.
Alisema, faharisi za jumla zilipungua hadi 116.7 mnamo Agosti 2021 ikilinganishwa na 114.3 iliyorekodiwa mnamo Agosti 2020.
Alizitaja bidhaa zilizochangia kupungua kwa kiwango cha mfumko wa bei ya mwaka ni mchele wa basmati (0.9%), mchele wa Mbeya (9.5%), unga wa mahindi (1.5%), ndizi za mtwike (1.9%), samaki (8.7%) na saruji (11.2%).
Mchumi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Ulrick Mbumbuvi, alisema, kushuka kwa mfumko kumechangiwa na kuwepo kwa bidhaa za kutosha kwenye masoko na uzalishaji mzuri.
Aidha, alisema, kuwepo kwenye tarakimu moja, ni njia bora ya kuwavutia wawekezaji kwa ajili ya kuwekeza nchini kwa ajili ya maendeleo ya taifa.
Mhadhiri wa Uchumi Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA), Dk. Stella Ngoma Hassan, alisema, bado hali inaonesha kuwa vizuri kiuchumi na kuleta faraja kwa wananchi na taifa kwa ujumla.