LONDON,UINGEREZA

MGOGORO wa uhaba wa nishati nchini Uingereza sambamba na kusababisha misururu na foleni ndefu za magari mbele ya vituo vya mafuta na msongamano mkubwa katika miji mbalimbali ya nchi hiyo, vilevile umesababisha mpagaraganyiko mkubwa katika sekta ya huduma za umma nchini humo.

Ripoti zinasema kuwa, maelfu ya wafanyakazi wa Uingereza wakiwemo wa huduma za umma, walilazimika kubakia majumbani mwao kutokana na uhaba wa mafuta baada ya asilimia 90 ya akiba ya mafuta ya petroli ya vituo vya mafuta vya miji mikubwa ya Uingereza kumalizika.

Jumuiya ya Vituo vya Mafuta nchini Uingereza imetangaza kuwa, vituo 5,500 vya mafuta nchini humo vimefungwa kutokana na ukosefu wa bidhaa hiyo.

Jumuiya hiyo imetahadharisha kwamba akiba ya vituo vyengine vya mafuta pia inaelekea kumalizika.

Olaf Scholz,Waziri wa Fedha wa Ujerumani alisema kuwa uhaba wa madereva wa malori na mafuta nchini Uingereza ni tatizo linalohusiana na uamuzi wa nchi hiyo kujiondoa katika Umoja wa Ulaya, Brexit.

Ripoti zinasema Uingereza inasumbuliwa na changamoto ya uhaba wa asilimia 90 ya madereva uliosababisha na Brexit na maambukizi ya virusi vya corona.