NA ABOUD MAHMOUD

WASWAHILI wana misemo yao kama vile ‘Udongo upate ulimaji au Samaki mkunje angali mbichi’, misemo hii ina maana nyingi.

Maana halisi ya misemo hiyo ni kumuandaa mtoto katika mafundisho mema na yaliyo bora, ambayo yatamfaa wakati akiwa mtu mzima.

Misemo hiyo imeweze kutumika kwa takriban miongo mingi na ukweli wake unaonekana miaka na miaka, kwani mengi wanayofunzwa watoto utotoni huwasaidia baadae.

Kwa wananchi wa visiwa vya Zanzibar tunakumbuka kila ifikapo Septemba 23 tunaadhimisha sherehe za elimu bila ya malipo, ambapo mwaka huu kilele chake kitakua siku ya Alhamis wiki ijayo.

Shamrashamra za kuadhimisha sherehe hizo tayari zimeanza na zinaendelea mpaka siku ya kilele chake inayotarajiwa kufanyika kisiwani Pemba.

Katika  shamrashamra za maadhimisho ya siku hiyo muhimu, tumeshuhudia michezo mbali mbali, ikiwemo soka, kikapu, netiboli, mashairi na mengine mengi ikifanywa na wanafunzi kutoka skuli mbali mbali.

Michezo hiyo pia tulishuhudia kuleta ushindani baina ya skuli na skuli  ambapo kila skuli ilionekana kujipanga vyema na kutaka kuondoka na ubingwa wa sherehe hizo.

Kiukweli ni jambo jema na zuri kwani kufanya hivyo kunasaidia kuibua vipaji vya michezo kwa vizazi vyetu vijavyo ambao watasaidia katika kukuza sekta za michezo.

Kutokana na hayo tulioyaona katika shamrashamra hizo ni wajibu wetu sote, kuhakikisha michezo katika maskuli iwe chachu ya kukuza sekta hiyo na kuifanya Zanzibar iwe maarufu katika ulimwengu wa michezo.

Ni jambo sahihi na lisilo na kipingamizi kwamba vijana wengi kwenye skuli zetu wapo wanaopenda michezo na wamekua wakifanya vizuri katika maeneo hayo.

Napenda kurudia tena kauli yangu ya mwanzo kuwa udongo upate ulimaji na samaki mkunje angali mbichi, maneno yangu haya yanafikia hapa.

Tayari vijana wetu tumefanikiwa kuwashirikisha katika michezo kwenye ngazi za maskuli, sasa hivi kilichobakia ni kuwaendeleza ili waweze kufika mbali na kuitangaza vyema nchi yetu.