NA ABOUD MAHMOUD

IDARA ya Michezo Zanzibar imejipanga kuhakikisha inaanzisha michezo mipya ndani ya mwaka huu, ili kuinua sekta hiyo na kuleta mafanikio zaidi.

Hayo yameelezwa na Kamishna wa Idara ya Michezo Zanzibar Ameir Mohammed Makame wakati akizungumza na Zanzibar Leo huko ofisini kwake uwanja wa Mao Zedong.

Kamishna huyo alisema lengo la kuanzishwa michezo hiyo ni kuhakikisha vipaji vyote vya michezo Zanzibar vinatumika inavyotakiwa.

“Tumeamua kuanzishwa michezo mipya ingawa michezo hiyo itakua mipya kwa hapa nyumbani, lakini sio nchi nyengine na mengine itakua mipya kote lengo letu ni kuhakikisha vipaji vya michezo Zanzibar vinatumika ipasavyo,”alisema.

Kamishna Ameir aliitaja michezo hiyo ni pamoja na nage ya ufukweni, Wood balls,Kabadia na Raga au kwa jina la umaarufu Rugby.

Aidha Ameir alisema Idara yake tayari imeanza kufanya mazungumzo na walimu wa michezo hiyo kwa lengo la kuwafundisha vijana wa Kizanzibari.

“Tayari tumeanza mazungumzo na walimu wa michezo hii na iani yangu kubwa michezo hii itasaidia kuitangaza vyema nchi yetu katika mataifa mbali mbali kupitia sekta ya utalii na uchumi wa buluu,”alifafanua.

Sambamba na hayo Ameir alitoa wito kwa wazazi kwa kuwaruhusu watoto wao kushiriki katika michezo, ambayo itawasaidia kujiepusha na maradhi, vikundi viovu na kupata ajira.