NA ASYA HASSAN
OFISI ya Rais Fedha na Mipango, imewataka wananchi kuwa makini wanapotumia kampuni za kuweka fedha, ili kujiepusha na utapeli.
Mkurugenzi Mipango, Sera na Utafiti Ofisi ya Rais na Mipango, Saumu Khatib Haji, akizungumza na vyombo vya habari katika zoezi la kuhakiki wa wafanyakazi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na wafanyakazi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), waliyoweka fedha zao katika kampuni ya Masterlife Microfinance Ltd.
Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango iliutangazia umma Agosti 3, ya mwaka huu kusitisha shughuli za kampuni hiyo baada ya kugundulika inaendesha shughuli zake kinyume na taratibu na sheria za nchi.
Hivyo kutokana na hatua hiyo serikali iliamua kuchukua hatua tofauti ikiwamo kukaa vikao tofauti na wawakilishi wa waathirika hao, viongozi wa kampuni hiyo na wadau tofauti na kuona ipo haja ya kufanywa uhakiki wa waathirika hao, ili ijiridhishe na hatimae kuweze kuchukuliwa hatua zinazostahiki.
Alisema Zanzibar hivi sasa kumeibuka kampuni nyingi za namna hiyo, hivyo ni vyema wananchi wanapotaka kuzitumia kampuni hizo wazichunguze ili kujiepusha kutapeliwa.
“Wapo baadhi ya wananchi huazisha kampuni hizo kwa maslahi yao binafsi, hivyo ni vyema wananchi kufanya uchunguzi kwanza kama chombo hicho kipo salama na sio kukurupuka kwenda kujiunga hali ambayo inaweza kusababisha kutokezea kwa athari kubwa hapo badae,”alisema.