NA MADINA ISSA

MKUU wa miradi kutoka taasisi ya Zanzibar Milele Foudation (ZMF), Khadija Ahmed Sharif, amesema sekta ya elimu inahitaji jitihada zitakazowawezesha wanafunzi kujifunza kulingana na wakati uliopo.

Aliyasema hayo, mara baada ya kufunguliwa kwa kambi ya siku tano ya kuwawezesha wanafunzi mbinu za ufundishaji kwa walimu wa skuli wa Unguja na Pemba, mafunzo ambayo yalifanyika katika Chuo cha Maendeleo kilichopo Dunga, wilaya ya Kati, mkoa wa Kusini Unguja.

Alisema, mafunzo kwa walimu huongeza kasi ya maendeleo ya elimu kwa kutumia sayansi na teknolojia katika skuli zao kwa kuona wanafunzi wanakuwa na wigo mpana wa uelewa na kuweza kufanya kazi zao za masomo kwa kila siku.

Alisema kuwa jitihada zaidi zinahitajika kati ya walimu na wadau mbali mbali katika kuendeleza sekta ya elimu nchini ili kuiwezesha nchi kukuwa kimaendeleo kupitia sekta hiyo.

Aidha allisema ni vyema walimu kuwa tayari kujifunza ujuzi wa aina tofauti ili kuwawezesha wanafunzi kufanikiwa.

“Tumekuwa tukitoa elimu mbali mbali kwa wanafunzi na kwa sasa tumekuja kwa walimu ili kuendana na karne ya 21 ili wanafunzi waweze kubuni, kufikiri pamoja na kutatua matatizo mbalimbali na kuwa wabunifu wa kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili,” alisema.

Alisema karne ya sasa wanafunzi wanahitaji kujua ujuzi wa kila aina ambapo walimu wanahitaji kuwatayatisha na uwepo wa mafunzo hayo, wataweza kuwafahamisha wanafunzi wao pamoja na kuandaa kambi kama hizo ili kuona wanapeleka mabadiliko katika skuli zao.

Aidha alisema kuwa mafunzo hayo, yaliwashirikisha walimu 100 waliopo katika mkakati wa taasisi hiyo kutoka wilaya za Unguja na Pemba ikiwemo, skuli ya Aboud Jumbe iliyopo Fuoni, Kinuni, kwa uande wa Pemba Chasasa, Fidel Castro na Mkanyageni.

Mkufunzi wa walimu hao, Shaaban Yussuf, alisema, katika karne iliyopo hivi sasa ni kujifunza ili kuendelea kuwafunza wengine kwa lengo la kujitafutia ajira kwa kufikiri mbinu mbalimbali.