NA TATU MAKAME

MAMLAKA ya Uhifadhi na uendelezaji Mji Mkongwe imewatahadharisha watumiaji na wakaazi wa mji huo kuacha kujihususha na uharibifu wa uhalisia wa majengo kwa kubadilisha milango ya asili, ili kuepuka kuharibu utamaduni wa wazanzibari.

Akizungumza katika hafla ya maonesho ya maswahili huko Forodhani Wilaya ya Mjini Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo Madina Haji Khamis, alisema ni vyema wananchi kutambua kuwa alama hiyo ni moja ya urithi wa dunia, hivyo kuendelea kutoa milango hiyo kunaweza kuathiri nchi hasa katika sekta ya Utalii ambayo ni miongoni mwa chanzo cha uchumi wa Zanzibar.

Alisema kumekuwa na utaratibu usiokubalika wa kubadilisha majengo hayo ikiwemo kutoa milango kwa visingizio tofauti na kuiuza ndani na nje ya nchi, ili kupata fedha na kubadilisha aina ya milango ya kisasa ambayo inapoteza haiba ya majengo hayo.

Hata hivyo, alisema kufanya hivyo ni kupoteza uhalisia wa majengo ambapo ni athari kubwa kwa urithi wa dunia.

“Wapo wanaosema nyumba zile ni za kishamba kwa kuwa milango yake ni ya mbao, kama wazazi wetu walianza kuitoa kipindi hicho tungejuwaje kama kulikuwa na aina ya utamadunmi wa milango”,alisema.

Alisema Mji huo, unatambulika kwa kuwa na milango ya asili lakini wamejitokeza baadhi ya wananchi wanaoishi katika mji huo kuuza milango hiyo na kuweka milango ya kisasa ya (Aluminiam) ambayo inapoteza uhalisia wa mji huo.

Akizungumzia kuhusu ukarabati wa Jumba la Beit Al Ajab Mkurugenzi huyo alisema mamlaka itahakikisha ukarabati wa jengo hilo unafanywa kwa kurejesha uhalisia wake ili kuendelea kutunza utamaduni wa dunia.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya uhifadhi Mji mkongwe Maryan Jaffar Ismail, amewataka wananchi wa Zanzibar kuendelea kuutunza utamaduni wa mswahili ikiwemo kutengeneza na kuuza bidhaa zenye asili ya Zanzibar, ikiwemo mikoba, mikeka na mavazi ili vizazi kutambua thamani ya utamaduni huo.

Zawadi Malik Mzee Kutoka Chuo kikuu cha Zanzibar (SUZA) alisema wameamua kuandaa maadhimisho hayo ili kuendeleza utamaduni wa siku ya utalii kwa kuonyesha mavazi kuendeleza utamaduni na kuisaidia jamii kufahamu utamaduni wa mswahili.

Maonesho hayo ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya utalii duniani ambayo kitaifa yanafanyika katika kisiwa cha Pemba yakiwa na kauli mbiu isemayo ‘utamaduni wetu ni urithi wetu’.