PORT-AU-PRINCE, HAITI

MJUMBE maalumu wa utawala wa rais Joe Biden nchini Haiti amejiuzulu kwa kupinga kufukuzwa bila kujali utu kwa wahamiaji wa taifa hilo pindi wanapoingia Marekani.

Haiti ni nchi ambayo imekumbwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe na majanga.Daniel Foote aliteuliwa kwenye uadhifa huo mwezi Julai, kufuatia kuuawa kwa rais Jovenel Moise.

Hata kabla ya kufukuzwa wahamiaji hao kutoka mji mdogo wa Texas wa mpakani Del Rio, mwanadiplomasia huyo anajulikana kama mtu aliyekerwa sana na ukosefu wa hatua za haraka kutoka Washington na uzembe katika juhudi za kuboresha hali nchini Haiti.

Foote alimuandikia waziri wa mambo ya nje Antony Blinken akimuelezea kwamba amejiuzulu mara moja, kwa masikitiko makubwa na kuomba msamaha wanaotaka mabadiliko muhimu.

Alisema mfumo wa sera kwa Haiti bado una kasoro kubwa, na mapendekezo ya sera yalipuuzwa na kutupiliwa mbali, au kuhaririwa na kutoa maelezo tofauti .

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imemkosoa Foote kwa kujiuzulu katika kipindi kigumu na imetupilia mbali madai kwamba mapendekezo yake ya sera yalipuuzwa.