NA HAMIS DAMBAYA

HIVI karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alizindua mkakati wa uelimishaji na uhamasishaji wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.

Katika mengi aliyoyaeleza kwenye hafla ya uzinduzi huo, alitoa wito kwa zoezi hilo kufanyika kwa uadilifu mkubwa ili takwimu zitakazopatikana ziweze kusaidia katika kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo.

Sensa ya watu na makazi ni muhimu sana katika kujua takwimu ambazo ndizo zitakazosaidia kujua hali halisi ya idadi ya watu na makazi katika nchi ili kupanga mipango sahihi ya maendeleo na hivyo kuisaidia serikali kujua namna bora ya kutekeleza mipango yake.

Uamuzi wa Ofisi za Takwimu ile ya Bara na Zanzibar wa kuzindua mkakati wa uelimishaji na uhamasishaji umekuja wakati muafaka hasa kwa kuzingatia uzoefu wa sensa za miaka ya nyuma ambapo zoezi kama hili lilikuwa halina mkakati mahsusi wa kuwafikia walengwa na hivyo kujikuta zoezi lenyewe likikumbana na changamoto mbalimbali kutoka kwa jamii.

Uzoefu wa mazoezi kama haya ulifafanuliwa vizuri na waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba ambaye siku ya uzinduzi alieleza kwa kina umuhimu wa mkakati wa uhamasishaji na uelimishaji kuwa ni jambo lenye manufaa kwani panapokuwa na zoezi kama hili hutokea baadhi ya vikundi ama mtu mmoja mmoja ambao huwa na mawazo hasi.

Dk. Mwigulu aliwatoa hofu wananchi kuhusiana na umuhimu wa sensa ya watu na makazi lakini pia akiahidi kutumia mkakati huo katika kuhakikisha kuwa wananchi wanapata uelewa juu ya umuhimu wa kuhesabiwa na katika sensa ya mwaka ujao itagusa maeneo mengi ambayo yote yana manufaa kwa wananchi wenyewe na taifa kwa ujumla.

Viongozi mbalimbali ambao walipata fursa ya kuzungumzia zoezi la uhamasishaji na uelimishaji hawakusita kutumia mbinu mbali mbali na mifano kadhaa wa kadhaa ilikuonesha umuhimu wa sensa ya watu na makazi kwa maendeleo ya taifa na na mwelekeo nzima wa uchumi wa Afrika na dunia kwa ujumla.

Kamisaa wa sensa kutoka Tanzania Bara, Spika mstaafu Anne Makinda aliwakumbusha wananchi kwamba sensa ni kama mama anapotaka kupika chakula ni muhimu kufahamu idadi ya watoto wake.

Hivyo, ili aweze kujua mahitaji yanayohitajika kabla hajafanya matayarisho ya chakula hicho, hii ikiwa na maana kwamba takwimu sahihi za watu ndio msingi wa taifa kufikia hatua ya maendeleo.

Kwa mujibu wa viongozi wa Ofisi za Takwimu Tanzania Bara na Zanzibar wameeleza mafaniko makubwa yaliyofikiwa katika sensa za majaribio zilizofanyika katika baadhi ya mikoa hapa nchini na kusisitiza kuwa sensa ya mwakani itakuwa ni ya aina yake kwani itafanyika kwa kutumia utaratibu wa kidigitali ambao utaweza kutoa matokeo ya sensa hiyo ndani ya mwezi mmoja.

Mtakwimu Mkuu kutoka ofisi ya Taifa ya Takwimu Dk. Albina Chuwa aliwaeleza watanzania waliokuwepo kwenye mkutano huo kwamba ana matumaini makubwa sana kazi hiyo itafanyika kwa ufanisi wa hali ya juu kutokana na serikali kuwa na utashi wa kisiasa katika kuhakikisha kuwa inapata takwimu sahihi ili iweze kutekeleza mipango yake ya kimaendeleo.

Dk. Chuwa ambaye ni mbobezi katika masuala ya takwimu ndani na nje ya Tanzania katika mkutano huo alionesha umahiri mkubwa katika kuzungumzia masuala ya takwimu jambo ambalo linatoa imani kwamba zoezi hili litapata mafanikio ambayo yatakuwa ni ya kupigiwa mfano.

Ni heshima kwa taifa kuingia katika sensa ya mwaka 2022 chini ya uongozi wa Dk. Chuwa ambaye ndiye Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu na   hii ni kutokana na kila anapozungumzia masuala ya sensa anadhihirisha kwamba yeye ni mtu wa kazi yenye matokeo.

Dk. Chuwa na pacha wake Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar, Mayassa Mahfudhi Mwinyi katika uzinduzi wa mkakati wa uelimishaji na uhamasishaji waliihakikishia dunia kwamba ofisi zao zimejipanga ili kuona kila mtanzania anashiriki katika zoezi hilo muhimu linalotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka 2022 na hivyo umahiri wao unadhihirisha wazi kuwa zoezi la sensa litakuwa na mafanikio makubwa.

Ndio maana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alizipongeza ofisi hizo na kueleza kufurahishwa kwake kutokana na uamuzi wa kuandaa mkakati wa uhamasishaji na uelimishaji ambapo kwa maneno yake alikiri kuusoma na kuuona una tija kubwa katika kufanikisha zoezi la sensa.

Katika hotuba yake Rais Samia alitoa wito kwa Ofisi hizo kuhakikisha kwamba zoezi la uhamasishaji na uelimishaji linapewa kipaumbele kwa kuhakikisha makundi yote katika jamii yanafikiwa ili kupata elimu ya zoezi hilo kitu ambacho kitasaidia kila mtu atakayekuwa amelala ndani ya Tanzania kuamkia siku ya sensa anahesabiwa.

Samia alisisitiza kuwa makundi yatakayotumika katika uelimishaji waifanye kazi hiyo kwa kuzingatia uzalendo na kuwataka watendaji katika zoezi la sensa kuhakikisha kwamba wanatumia rasilimali wanazopatiwa katika kufanikisha zoezi hilo kwa umakini ili kuepuka kutumia fedha nyingi na rasilimali nyingi.

Ushauri huo Rais Samia wakati huu tunapoelekea katika zoezi la uhamasishaji na uelimishaji jamii una umuhimu mkubwa hasa ukizngatiwa uzoefu uliopatikana kupitia sensa za miaka ya nyuma ambapo kukosekana kwa mbinu sahihi za kutoa elimu kulisababisha zoezi la sensa kukumbwa na changamoto kadhaa ikiwemo baadhi ya watu kugoma kuhesabiwa.

Kwa mfano sensa ya mwaka 2012 ilikubwa na changamoto ya baadhi ya watu kugomea maswali yaliyopo kwenye dodoso na hivyo kikundi hicho cha watu kuhamasisha wanaowaunga mkono kutoshiriki katika zoezi hilo jambo ambalo liliathiri matokeo ya sensa yenyewe.

Katika uzinduzi wa mkakati wa Uhamasishaji na Uelimishaji Ofisi za Takwimu zilianza vizuri kwani katika mkutano huo ilionekana ushiriki wa makundi yote ambayo yalialikwa hivyo kutoa taswira kubwa kwamba kwa sensa ya mwakani hakutakuwa na watu watakaopotosha zoezi hilo hasa ikizingatiwa mkakati wenyewe umeanza mapema.

Kilichobaki kwa sasa ni kwa watakwimu wakuu wa sensa pande zote mbili za Tanzania kuyatumia makundi hayo vizuri kwa kuwapatia elimu ya kutosha kuhusiana na umuhimu wa zoezi la sensa na ofisi hizo zinatakiwa kutumia njia rahisi ambazo kila mtu atazielewa.

Katika uelimishaji ni vema pia Ofisi za Takwimu zikawatumia wanafunzi katika ngazi mbalimbali kwa kuandaa nyimbo, mashairi, ngonjera na hata ngoma kwani kundi la wanafunzi lina watu wengi nyuma yao na linaweza kutumia maarifa ambayo wanayapata kuhusu sensa na kuwaelimisha wazazi.

Itakumbukwa miaka ya nyuma kulikuwa na mashindano mbalimbali ya kuelimisha jamii kuhusu sensa yaliyofanyika katika ngazi ya skuli za msingi, sekondari pamoja na vyuo ambayo bado yanaweza kufanyika tena kwa gharama rahisi na hivyo kuboresha zoezi lenyewe na hapo itatumia fursa kwa kundi hilo nalo kutimiza wajibu wake.

Ni jukumu la Ofisi za Taifa za Takwimu kuhakikisha hawatumii tu wasanii wa kizazi kipya katika uelimishaji na uhamasishaji ambapo katika zoezi la uzinduzi wa mkakati wenyewe imeonesha wazi wasanii hao kushindwa kuubeba ujumbe wa sensa na badala yake kutumbuiza nyimbo zao wanazoziimba kila siku jambo ambalo halileti tija kwa hadhira.

Ni vema Ofisi hizo zikatumia pia bendi za muziki wa dansi na taarab katika kuwapa maelekezo mahsusi ya kutunga nyimbo zenye maudhui ya sensa ili katika vyombo vya habari na mikutano ya aina hiyo zitumike nyimbo hizo katika kutoa elimu kwa wananchi jambo ambalo litayafanya masikio ya watu kujua kwanini nchi inaelekea kwenye zoezi la sensa.

Makundi mengine ambayo ni muhimu yakapewa kipaumbele katika kuelimisha na kuhamasisha jambo hili ni pamoja na viongozi wa dini mbalimbali, viongozi wa jadi, vyombo vya habari, makundi ya wakulima na wafugaji ambao nao kupitia taasisi zao wanaweza kuifanya kazi hii kwa umahiri mkubwa kama ilivyopendekezwa kwenye mkakati wenyewe.

K wa mfano vyombo vya habari kwa kutumia vipindi vinavyogusa makundi mbalimbali vinaweza kutumika vizuri ikiwa Ofisi hizi za Takwimu zitaweza kuvishirikisha na kuchagua vionjo ambavyo vikiandaliwa kwa umahiri na ustadi vitaweza kuwavuta wananchi kusikiliza hasa kundi la vijana ambalo linahitaji umakini mkubwa ili kufikiwa na vyombo vya habari.

K wa ujumla uhamasishaji na uelimishaji ni jukumu kubwa na nyeti hivyo ni busara kuhakikisha kwamba kila mtu anapata elimu kuhusu zoezi lililo mbele ya taifa la watu kuhesabiwa hivyo ni vema kila mmoja katika taifa kuhakikisha anatumia maarifa yake katika kuwafikia wananchi.

Kama alivyosema mheshimiwa Rais Samia kipindi kilichobaki kinatosha kabisa kuifanya kazi ya uhamasishaji na uelimishaji na hivyo katika zoezi hilo la sensa kuhakikisha kila mtu anahesabiwa kwani zinapopatikana takwimu sahihi itasaidia taifa kupanga mipango yake kwa kujiamini na mwisho wa siku kusaidia kupatikana kwa maendeleo.

Ni matumaini makubwa kwamba kuzinduliwa kwa mkakati huu na kama utatekelezwa kama ilivyokusudiwa lengo la serikali litafikiwa kwa kuhakikisha katika sensa ya mwaka ujao hakuna mtu ambaye ataachwa na kwa kufanya hivyo taifa litakuwa linajua idadi sahihi ya watu wake pamoja na majengo jambo ambalo litasaidia utekelezaji wa mipango mbali mbali ya serikali kuwa rahisi na kutekelezwa kwa ufanisi.

Ni matumaini ya kila mtanzania kwamba ofisi zote za Takwimu kwa sasa zimejifunga mkaja katika kuhakikisha kuwa mkakati huu unatekelezwa kwa kasi na umahiri mkubwa jambo ambalo ndiyo litakuwa nguzo ya matokeo yanayotarajiwa kupatikana katika zoezi lenyewe la sensa linalotajiwa kufanyika hapo mwakani.

Mwandishi wa Makala hii anapatikana kupitia namba 0713 292741