NA ASIA MWALIM

TAASISI mbali mbali zilizopo nchini zimetakiwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha wanakuza kiwango cha ufaulu wa wanafunzi hapa nchini.

Mkurugenzi Idara ya Maendeleo Vijana Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo, Shaib Ibrahim Mohammed, alitoa wito huo alipofungua mkutano wa Taasis ya Zanzibar Vission Development Organization (ZAVIDO) hafla iliyofanyika skuli ya Mwanakwerekwe ‘C’ Zanzibar.

Alisema kufanya hivyo kutasaidia kufikia lengo la Serikali katika kufanikisha juhudi za kuimarisha maendeleo ya elimu kwa kuoengeza viwango vya wanafunzi wanaofanya vizuri kwenye mitihani ya ndani na taifa.

Aidha, alisema Wizara kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ya elimu inatoa fursa mbali mbali kutokana na kuwagusa zaidi vijana pia itaendelea kuunga mkono taasisi hiyo kuona kampeni ya elimu inafikiwa kwa kiwango cha juu.

Alifahamisha kuwa wizara imeamua kuunga mkono taasisi zenye lengo la kukuza ufaulu kwa vijana wa sekondari na wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani ya taifa ikiwemo kidato cha pili, kidato cha nne na sita, hivyo alizitaka taasisi nyengine kulipa kipaombele suala hilo.

Mapema Mkurugenzi huyo, alisema taasisi zina michango mikubwa katika kuisaidia serikali kufanikisha maendeleo hivyo wanapaswa kutoa kipaombele kwenye suala la upatikanaji na kuboresha viwango vya elimu hapa nchini.

Nae Naibu Katibu Mkuu Jumiya ya ZAVIDO, Khatib Hamad Kombo alisema kutokana na changamoto walizogundua kwa wanafunzi kupelekea ufaulu mdogo wameamua kuhamasisha wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani ya taifa, ili kujua thamani ya wanachokifanya kwenye masomo yao kabala ya kumaliza masomo.

Aidha alisema jumuiya ipo karibu sana na wanafunzi na kutooa taaluma mbalimbali ikiwemo mbinu za ufaulu, maadili ya kujenga heshima na nidhamu ambayo ni msingi wa mafanikio.

Hata hivyo, alishukuru serikali kuunga mkono taasisi hiyo kuhakikisha inafikia malengo husika na kutoa michango ya kuinyanyua kupitia wadau wa taaluma hiyo hivyo waliahidi kufikia maendeleo ya kielimu hapa nchini na kuwataka wanafunzi kuitumia elimu hiyo kipindi cha mitihani na baada ya mitihani.