VIENNA, AUSTRIA

MKUTANO wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, IAEA umeanza mjini Vienna nchini Austria.Nchi wanachama zinatarajiwa kujadili masuala ya hivi karibuni ya nchini Iran na Korea Kaskazini.

Iran ilizidisha urutubishaji wa urani tangu Marekani ilipojiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya 2015 na kuiwekea tena Iran vikwazo.

Akizungumza na wanahabari, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA Rafael Grossi alielezea mashaka juu ya hali ngumu inayolikabili shirika lake katika kufuatilia mpango wa nyuklia wa Iran.

Wakati wa ziara yake ya hivi karibuni nchini Iran, Grossi alipata idhini ya wakaguzi wa IAEA kuziangalia kamera za ufuatiliaji zilizo kwenye vituo vya nyuklia vya Iran.

Lakini Iran haikuliruhusu shirika hilo kufanya ukaguzi wa kushtukiza.

IAEA pia ilielezea mashaka makubwa kuhusiana na shughuli za uendelezaji wa nyuklia nchini Korea Kaskazini.

Katika ripoti yake ya hivi karibuni, shirika hilo lilisema kuna dalili kuwa Korea Kaskazini ilianzisha tena shughuli za kinu cha nyuklia mjini Nyongbyon mapema mwezi Julai.