NA MADINA ISSA

MKUTANO wa nne wa Baraza la 10 la Wawakilishi unatarajiwa kuanza Septemba kesho, kwa shughuli mbali mbali ikiwemo maswala na majibu yataulizwa na kujibiwa.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari katika ukumbi mdogo wa Baraza la Wawakilishi, Chukwani jana, Katibu wa Baraza hilo, Raya Issa Mselem, alisema jumla ya maswali 150 yatawasilishwa na masuala 115 yatajibiwa huku masuala 35 yatakayobakia yatapatiwa majibu katika mkutano ujao.

“Mkutano huu utakuwa mfupi sana hivyo, kati ya masuala 150, masuala 115 pekee ndiyo yatakayojibiwa katika kikao kinachokuja,” alisema.

Alifahamisha kuwa kikao hicho kinatarajiwa kuchukua wiki mbili na kumalizika Septemba 17 ambapo katika kipindi hicho miswaada ya sheria itawasilishwa na kusomwa kwa mara ya pili ambayo imeshasomwa katika mkutano wa mwezi Mei 2021.

Aliitaja miswaada yenyewe kuwa ni pamoja na mswada wa kuanzishwa kwa Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar na kuweka usimamizi mzuri wa shughuli za kiislamu Zanzibar na mambo mengine yanayohusisana na hayo.

Raya aliutaja mswaada mwengine kuwa ni wa marekebisho ya sheria mbali mbali na kuweka masharti bora ndani yake na mswaada wa sheria ya kuanzisha Ofisi ya Msajili wa Hazina na Usimamizi wa mali za umma na mambo mengine yanayohusiana na hayo.

Sambamba na hayo, alisema kuwa kutatolewa taarifa ya serikali kuhusu suala la ukodishwaji wa nyumba inayotumika kwa ajili ya vipimo vya covid 19 Mazizini, na taarifa ya serikali kuhusu mtumishi wa serikali kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kupitia kitengo cha benki ya damu

Taarifa nyengine itakayotolewa ile ya kamati ya Maadili na Kinga za wajumbe kuhusu malalamiko dhidi ya mjumbe wa baraza hilo, Ali Suleiman Ameir kutoka kwa Dk. Hassan Rashid Ali.