KABUL, AFGHANISTAN
KUNDI la Taliban limeahidi kuhakikisha usalama wa wafanyakazi wanaotoa misaada ya kiutu na wa usambazaji wa misaada hiyo nchini Afghanistan.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric,alisema hayo kupitia taarifa baada ya kundi hilo kukutana na Mkuu wa utoaji misaada wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths.
Griffiths amekuwa akifanya vikao kadhaa mjini Kabul na alikutana na viongozi wa Taliban wakati kuna kitisho cha kutokea mgogoro wa kibinadamu nchini humo chini ya uongozi mpya wa kundi lenye misimamo mikali ya kidini.
Ripoti imeongeza kuwa Griffiths alisisitiza kwamba watoaji misaada walijitolea kuhakikisha wanawahudumia ipasavyo watu wenye mahitaji bila ya upendeleo.
Griffiths alitilia mkazo haja ya kuhakikisha haki na usalama wa wanawake unalindwa, wakiwemo raia na watoaji misaada.
Chini ya iliyokuwa utawala wa Taliban kati ya mwaka 1996-2001 nchini Afghanistan, haki za wanawake zilikiukwa zaidi.