ROME, Italia
KOCHA, Jose Mourinho, aliikosoa timu yake kwenye ushindi wa magoli 5-1 dhidi ya CSKA Sofia, ukiwa ni ushindi wa sita mfululizo tangu achukue mikoba ya kuinoa AS Roma msimu huu.
Mourinho alikuwa mkali baada ya dakika ya 10 tu timu yake kuruhusu goli, huku ikiwachukua dakika 15 kusawazisha kupitia Lorenzo Pellegrini.
Ingawa, Mourinho hakuridhizishwa na kiwango cha timu yake, lakini, alimsifia nahodha wake, Pellegrini na kufichua siri kuwa atasaini mkataba mpya na timu hivi karibuni.
Mourinho alinukiliwa akisema:”Siku mbili zilizopita tulifanyia mazoezi hili, lakini, mabeki hawakufanya hivyo, hawakuwa na waledi wa kutosha, walipoteana”.
“Siwezi kusema tulicheza vibaya, ila hatukufanya vizuri na hakika ushindi wa 5-1 haukutosha, ndio sisi ni bora kuliko CSKA Sofia, lakini hatukufanya juhudi za kutosha”.
Magoli ya Roma yalifungwa na Lorenzo Pellegrini aliyefunga mawili, Stephan El Shaarawy, Gianluca Mancini, huku Tammy Abraham akifunga goli la mwisho na goli pekee la CSKA-Sofia lilifungwa na Graham Carey. (AFP).