KINSHASA, DRC
RAIA wanne wameuawa na wengine kutekwa nyara Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo baada ya watu wanaoshukiwa wanamgambo wa kiislamu kuvamia msafara wa magari ya kijeshi na kuyachoma moto.
Serikali ilisema kwamba tayari wanajeshi wake wameokoa zaidi ya watu 50 miongoni mwa waliotekwa nyara kwenye jimbo la Ituri na kwamba operesheni za kuokoa wenzao waliobaki zinaendelea.
Kundi la ADF, lenye mizizi yake nchini Uganda linashukiwa kutekeleza shambulizi hilo kulingana na wizara ya mawasiliano ya Congo.
Hata hivyo Wizara hiyo haijasema ni watu wangapi waliotekwa nyara ingawa mbunge mmoja kutoka jimbo hilo awali alisema kwamba walikuwa takriban watu 80.
Msafara ulioshambuliwa unasemekana kuwa wa takriban magari 100 yaliokuwa yakilindwa na jeshi wakati yakisafirisha watu na bidhaa kati ya miji ya Beni na Butembo.
Mashambulizi kutoka kwa makundi yenye silaha mashariki mwa Congo kwenye mpaka na Rwanda na Uganda yamekuwa yakiendelea licha ya serikali kuweka utawala wa kijeshi kwenye majimbo ya Ituri na Kivu kaskazini mwanzoni mwa mwezi Mei.
Watu walionusurika kwenye mashambulizi hayo walisema risasi zilirushwa kutoka kila pande wakati baadhi ya magari yakiteketezwa muda mfupi baadaye.