NA LAYLAT KHALFAN

JAMII imeshauriwa kuacha matumizi ya vyuma wakati wakitumia huduma ya umeme na badala yake watumie vitu asili wakati wakitayarisha vyakula majumbani mwao vikiwemo mwiko na pawa za zinazozalishwa na mbao, ili kuepusha hatari zinazoweza kujitokeza.

Ofisa Mawasiliano wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), Haji Juma Chapa, aliyasema hayo Bumbwini katika Kijiji cha Kiyongwe Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja, wakati akitoa elimu ya kujiunga na huduma ya umeme sambamba na utumiaji mzuri wa huduma hiyo ili kujikinga na madhara yanayoweza kujitokeza.

Alisema watu wengi tayari washapata madhara mbalimbali na wengine kupoteza maisha kutokana na kutotumia huduma hiyo kwa uangalifu na kusababishia kukumbwa na kadhia hiyo.

“Tunapotumia vitu vya chuma wakati wakutumia nishati ya umeme tujitahidi kujiepusha na majimaji mwilini wakati wa kupika na kuvaa viatu kwa ajili ya usalama wetu”, alisema Chapa.