NA MADINA ISSA

MUFTI Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaabi, ameongoza viongozi wa dini mbali mbali kupata chanjo ya ugonjwa wa uviko 19 ili kujikinga na ugonjwa wa corona.

Akizungumza na waandishi wa habari mara ya kupatiwa chanjo hiyo, sheikh Kaabi, aliwataka wananchi kujitokeza kufanya hivyo ili kuunga mkono juhudi za serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo ulioikumba dunia toka mwishoni mwa mwaka 2019.

Kiongozi huyo akiwa na viongozi wenzake, walifika katika kituo cha kutolea chanjo hiyo kilichopo katika hospitali ya rufaa ya Mnazimmoja majira ya saa 5 asubuhi, wakifuatana na baadhi ya waumini wa dini zao.

Alisema endapo watakapopiga chanjo hiyo wataweza kuepukana na tatizo hilo, jambo ambalo dini inatoa kipaumbele kwa watu kujikinga dhidi ya maradhi na athari zake.

Aidha alisema kujikinga ni bora kuliko tiba, kwani ukijikinga unajiepusha na maradhi yenyewe ambapo inaepusha pia gharama wakati wa tatizo lishakufika.

“Tukijikinga tunaepusha gharama za matibabu hivyo nawaomba waumini wa dini zote tujitokezeni kwa wingi kupata chanjo ili kuepuka matatizo baadae,” alisema.

Alisema pamoja na kuwa kuchanja ni jambo la hiyari, viongozi hao kuwa mfano kwa lengo la kuunga juhudi za serikali kupambana na ugonjwa huo.

Hivyo, aliwataka waumini wote kwenda kufuata kinga hiyo kwani ugonjwa huo una madhara na yamekuwa yakiambukiza kwa kasi lakini wakijinga na kuendelea kuchukua tahadhari kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya ili taifa liwe na watu wenye afya bora.

Naye, padre Anselmo Mwang’amba, kutokea kanisa katoliki Parokia Kitope Zanzibar, alisema ameamua kupata chanjo hiyo baada ya kutambua umuhimu wake na kuzishukuru serikali za Tanzania kuweka utaratibu mzuri wa kupatikana kwa chanjo hiyo.

Hivyo aliwataka wananchi na waumini wengine waliokuwa tayari kujitokeza kwa wingi kuchanjwa, pamoja na kuendelea kuchukua tahadhari inayotolewa na wataalamu wa afya ikiwemo kuvaa barakoa, kuepuka mikusanyiko ili kuepukana na maradhi hayo.