NA ASYA HASSAN

MWAKILISHI wa Jimbo la Malindi, Mohammed Ahmad Salum, amesema ataendelea kuisaidia sekta ya elimu, ili kuhakikisha watoto wa jimbo hilo wanafanya vizuri hasa katika mitihani ya taifa.

Ahmada alisema hayo katika viwanja vya skuli ya Hurumzi alipokua katika hafla ya kukabidhi vifaa mbali mbali vya skuli ziliyopo ndani ya jimbo hilo pamoja na sare za skuli kwa watoto 85 waliokuwa wakiishi katika nyumba iliyoungua moto huko Kiponda Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Alisema elimu ni rasilimali muhimu hivyo atahakikisha anatoa kipaumbele katika kuwekeza kupitia sekta hiyo, ili kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi hao, ikiwa hatua itayosaidia kupata wataalamu wa ndani waliobobea kupitia fani mbali mbali.

Sambamba na hayo alifahamisha kuwa serikali  kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wa maendeleo nchini wamekua mstari wa mbele katika kuboresha mazingira ya elimu ikiwemo majengo ya kisasa, vifaa vya maabara na kuongeza idadi ya walimu wa kusomesha.

Alisema atahakikisha anaunga mkono jitihada hizo, ili kufikia malengo ya kuinua kiwango cha ufaulu kwa watoto hao na kuzithamini juhudi hizo, ili waweze kufanikiwa katika masomo yao.

Mwalimu Mkuu wa skuli ya Hurumzi, Wahida Hassan Haidar, alimshukuru kiongozi huyo kwa kujitolea kwake katika kuiunga mkono serikali kupitia sekta hiyo kutokana na eneo hilo ndio chachu ya kufanikisha shughuli mbali mbali za kimaendeleo.

Nae mwanafunzi wa skuli ya Kiponda, Yassir Hassan Vuai, alimuomba kiongozi huyo kuwasaidia kupata vitabu kutokana na viliyopo ndani ya skuli hiyo havikidhi mahitaji ya masomo yao, ikiwa pamoja na huduma ya maji kwa vile yaliopo hayoko salama kwa matumizi ya binadamu.

Baadhi ya wazee wa wanafunzi waliyopatiwa msaada wa walimshukuru Mwakilishi huyo kwa kuwapatia msaada huo na kumuomba awasimamie na kuwasaidia kupata vyeti vya kuzaliwa pamoja na vitambulisho vya taifa.