NA HAFSA GOLO
CHANGAMOTO ya kupasuka kwa kuta za baadhi ya madarasa skuli ya Jang’ombe Msingi na kukosekana uzio zimeleta hofu kwa walimu ya kuhatarisha usalama wa wanafunzi.
Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Jang’ombe”B” Msingi, Jabiri Mzee Mikidadi, alieleza hayo wakati alipokuwa akizungumza na gazeti hili ofisini kwake skulini hapo.
Alisema hofu hiyo imekuja kufuatia kukatika kwa viwambaza vya jengo lenye madarasa sita ambayo wanasomea wanafunzi 600 kwa siku.
Aidha alisema miongoni mwa vyanzo vilivyochangia kupasuka kwa madarasa hayo ni pamoja na ukosefu wa kutokidhi viwango vya ujenzi wa madarasa hayo, ambayo yalijengwa kupitia nguvu za wananchi pamoja na kutuama kwa maji ya mvua katika jengo hilo yaliosababisha mmomonyoko wa ardhi eneo hilo.
“Mvua kubwa zinaponyesha maji hutuama katika kiwambaza cha jengo hilo kutokana na hayana kwa kwenda baada ya kuzibwa kwa mtaro katika eneo hilo”,alisema.
Alisema ukosefu wa uzio skulini hapo ni tatizo sugu lililodumu muda mrefu na linaendelea kuleta athari ikiwemo ajali holela za wanafunzi zinazotokea ndani ya skuli.
Alifahamisha moja ya changamoto zinazojitokeza kutokana na ukosefu wa uzio na zinaleta wakati mgumu kwa walimu wa skuli hiyo alisema, wanafunzi zaidi ya wawili kwa mwezi hugongwa na wenye bodaboda wakiwa katika mazingira ya skuli.
“Bodaboda zinapita ndani ya maeneo ya skuli na zinaendelea kuleta athari huu mwezi uliopita watoto wawili waligongwa tukawapeleka hospitali hivyo tumewaita viongozi wa jimbo tukakaa nao nao wakaahidi kutatua kero hizo ikiwemo kuweka kifusi katika eneo linalotuama maji”,alisema.