NA SALUM VUAI

LICHA ya kuanza vizuri, mradi wa kuwarudisha madarasani watoto walioacha skuli kwa sababu mbalimbali, bado unahitaji msukumo na ushirikiano zaidi kutoka kwa wazazi, walezi na jamii kwa jumla.

Katika ziara iliyofanywa Septemba 21, 2021 na timu ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali inayoratibu mradi huo katika skuli tatu za Unguja, imebainika kuwa, changamoto kubwa iliyopo, ni uelewa mdogo wa wazazi juu ya umuhimu wa elimu.

Akizungumza na waandishi wa habari waliofika katika skuli ya msingi Fukuchani Wilaya ya Kaskazini ‘A’, Mwalimu Mkuu Khamis Mcha Khamis, alisema bado kuna watoto wengi nje ambao waliacha masomo au hawakuandikishwa kabisa walipotimiza umri wa kuanza skuli.

Hata hivyo, alifahamisha kuwa skuli yake imeupokea kwa furaha mradi huo, wakiamini utawakomboa watoto kielimu, na kusema walipopata taarifa, walishirikiaaa na masheha kuwakusanya na kuwahamasisha kurudi skuli.

Aidha aliihimiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kupitia waratibu wa mradi huo wa miaka mitatu, kuwatatulia changamoto za vifaa vya kufundishia na kujifunza, sambamba na posho za walimu ambao kimsingi si waajiriwa ingawa wamepata mafunzo ya ualimu.

Mwalimu mkuu huyo alieleza matumaini yake kuwa, kwa kuwepo ushirikiano na kutimiziwa mahitaji na waratibu wa mradi, mafanikio yatapatikana katika kipindi kifupi kijacho, kwani walimu pamoja na masheha wamejidhatiti kuwatafuta watoto wengine walioacha masomo na kila wiki idadi inaongezeka.

Tatu Ame Suleiman, Mwalimu Mkuu wa skuli ya  msingi Uzini alisema, katika darasa la elimu mbadala wamepata wanafunzi 20, na kuongeza kuwa milango iko wazi kwa wengine walioko mitaani ambao kwa kushirikiana na masheha na jamii, wanaendelea kuwafuatilia na kuwashajiisha.

Mratibu wa Idara ya Elimu Mbadala na Watu Wazima Wilaya ya Magharibi ‘A’ Ukasha Hamdu Juma, alisema skuli ya Mtopepo imekusanya watoto 39, na kwamba  hatua hiyo imewapa afueni kwani bila hivyo, baada ya muda mfupi watoto hao wangeweza kuangukia katika vikundi viovu na kujenga utukutu.