MINSK, BELARUS

KIONGOZI wa upinzani Belarus, Maria Kolesnikova amehukumiwa kifungo cha miaka 11 jela.Vyombo vya habari vya Belarus vinaripoti kuwa hii ni baada ya kuhusika katika maandamano ya mwaka jana kufuatia uchaguzi uliokumbwa na utata nchini humo.

Mshirika wa Kolesnikova ambaye pia ni wakili Maxim Snak alihukumiwa miaka kumi jela.

Wote wawili walihukumiwa kwa jaribio la kuchukua madaraka kinyume cha sheria.

Kolesnikova mwenye umri wa miaka 39 alikuwa nguvu kuu katika maandamano hayo yaliyokuwa yanampinga Rais Alexander Lukashenko.

Aliwahi kumfanyia kazi mgombea wa urais wakati mmoja Viktor Babariko na alitekwa nyara na jeshi la Belarus mjini Minsk mapema mwezi Septemba mwaka jana.