MUZNAT HAJI, SCCM

Wakaazi wa Mwanakwerekwe wamelalamikia  kero ya utupwaji taka ovyo katika mitaro ya maji, jambo ambalo linaonekana kuwa chimbuko la maradhi ya mripuko katika maeneo hayo.

Wakizungumza na Zanzibar Leo wakaazi hao walisema kuwa kitendo cha utupaji wa taka kiholela katika mitaro linasababisha athari za uharibifu wa mazingira hasa katika kipindi cha mvua.

“Watu wanatupa taka katika mitaro na hawaangalii chakutupa hasa zinaponyesha mvua uchafu unaongezeka na kunazagaa mitaani” alisema.

Aidha, wakaazi hao walisema kuwa kitendo hicho pia kinasabisha mitaro kuziba na kutokuwa na uwezo wa kupitisha maji kama inavyo takiwa kitendo ambacho kinaweza kupelekea maradhi ya mripuko kama kipindupindu na matumbo ya kuharisha katika maeneo hayo.

“Tatizo kubwa lipo kwetu sisi wananchi kila kitu tunatupa katika mitaro ya maji bila kujua kuna matatizo ambayo yanaweza kutupata’ walifahamisha  wakazi hao.

Hata hivyo wakaazi hao hawakuacha kutoa wito kwa jamii juu ya kuachana na tabia hiyo, ili kupunguza wimbi la maradhi ya mripuko katika jamii.

Diwani wa wadi ya Mwanakwerekwe, Fatma Juma Jabu, ambae pia ni Naibu Meya Manispaa ya Wilaya ya Magharibi ‘B’ alisema kuwa wakishirikiana na kamati ya shehia  tayari wamefanya juhudi za kuweka mikakati na sheria  ndogo ndogo  katika kuhakikisha wanaondoa tatizo hilo.

“tunashirikiana na kamati ya shehia katika kuhakikisha tunaitatua changamoto hii kwani inaonekana kushika kasi” alifahamisha diwani huyo.

Naibu Meya huyo, aliitaja mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa yeyote ambae ataonekana akifanya kitendo hicho kuchukuliwa hatua ya kusafisha mtaro husika pamoja na kulipa faini Manispaa, ili kusaidia kutatua changamoto hiyo katika maeneo hayo.