Asema serikali kuwahudumia wananchi wote

Aahidi kutatuliwa kero za maji, umeme

Waliovunjiwa kupisha barabara kuramba fidia

NA MARYAM SALUM, PEMBA

RAIS wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema serikali anayoiongoza itaendelea kuwatumikia wananchi wa Zanzibar na kuhakikisha inawaondolea kero mbali mbali zinazowakabili.

Hayo aliyaeleza jana huko katika kijiji cha Mleteni wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba, wakati akizungumza na wananchi wa kijiji hicho ikiwa ni muendelezo wa ziara yake kisiwani humo kuangalia miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi.

Alisema serikali ina dhamira ya kuyatekeleza hayo kwani ilishawaahidi wananchi wakati alipokuwa akiomba ridhaa ili waweze kumchagua kuwa rais wa awamu ya nane na kuwasihi wawe na subra.

Dk. Mwinyi aliwaeleza wananchi hao kuwa amezisikia kero zao na kuahidi kuzitatua sambamba na kuchangia shilingi milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa skuli ya maandalizi Mleteni na Mashuga ili kuunga mkono juhudi za wananchi walioanza ujenzi wa madarasa ya skuli kwa nia ya kuendeleza elimu kwa watoto wao.

Dk. Mwinyi, alitoa agizo kwa wizara ya Afya kuhakikisha huduma za uzazi zinaanza mara moja katika kituo cha Afya Kisiwani kwa Bint Abeid, ambapo vifaa vya kutoa huduma hiyo viko tayari.

Aidha aliitaka wizara ya Afya kufanya kila linalowezekana ili kuona wanakipatia kituo cha afya japo huduma ya mwanzo kwa kuanzia ili wananchi hao waweze kupata huduma hiyo muhimu.

Dk. Mwinyi, amekuwa kiongozi wa mwanzo mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kufika katika kijiji hicho tangu mwaka 1969 na hivyo amefarajika kutokana na mapokezi ya wananchi hao.

Nao watendaji wakuu wa Shirika la Umeme (ZECO), Mkurugenzi wa Wizara ya Uvuvi na Uchumi wa Buluu na Mamlaka ya Ujenzi wa Barabara, walimhakikishia Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kuzipatia ufumbuzi kero zote zinazowakabili wananchi wa kijiji cha Mleteni.

Wakati akijibu changamoto za makundi maalumu huko Kinyasini Pemba, Dk. Hussein Ali Mwinyi alisema amesikia kilio cha makundi hayo na kuwaahidi kuyafanyia kazi kwa kutafuta mbinu mbali mbali zitakazosaidia makundi hayo kujiendeleza zaidi.