NA JOSEPH NGILISHO, ARUSHA

NABII wa Kanisa la The Power of Perfection Ministry (nguvu ya utimilifu), Jackson Ibrahim (30) mkaazi wa jiji la Arusha amepandishwa kizimbani katika mahakama ya hakimu mkazi Arusha, wilayani Arumeru akidaiwa kubaka mtoto wa miaka 15 (jina limehifadhiwa).

Mwendesha mashtaka wa serikali, Blandina Msawa alidai mbele ya hakimu Patricia Kisinda kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo kinyume cha kifungu no 130 (1) (2) (A) na (131) (1) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwakan2019.

Msawa alisema Jackson Ibrahim anayekabiliwa na kesi ya jinai no 109 ya mwaka 2021, ilidaiwa mnamo Juni 18 mwaka huu katika eneo la majengo, jijini Arusha mtuhumiwa alimbaka msichana mdogo mwenye umri wa miaka 15 kinyume cha sheria.

Mshitakiwa mara baada ya kusomewa mashtaka hayo alikana na yupo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti Kwa kuwa na wadhamini wawili wenye mali zisizohamishika zenye thamani ya sh. Mil 10 kila mmoja.

Aidha makakama ilitoa masharti kwa Ibahimu ya kutotoka nje ya Mkoa wa Arusha bila kuwa na kibali cha mahakama na kesi hiyo imepangwa kutanjwa tena tarehe 13.10.2021.