NAOMI Osaka mcheza tennis aliyekwenye anga za juu duniani kwenye ubora wa wacheza tennis wanawake ambapo kwa sasa anashikilia mbari mbili ya ubora duniani.

Naomi alizaliwa miaka 23 iliyopita ambapo ilikuwa Oktoba 16 katika mji wa Chūō-ku, mama yake ni mjapani Tamaki Osaka na baba yake ni Leonard François mtu mweusi mwenye asili ya nchini Haiti.

Naomi ana dada yake anayeitwa Mari, ambaye pia ni mcheza tennis wa kulipwa, hata hivyo walipewa majina ya ukoo wa mama yao Osaka.

Leonard François na bi Tamaki Osaka walikutana na kufungua ukurasa wa mapenzi baina yao wakati Leonard François alipokuwa katika chuo cha Hokkaido kilichopo Japan.

Naomi akiwa na miaka mitatu familia yake ilihamia nchini Marekani katika jiji la New York, ambapo aliishi na baba yake ambapo baada ya kukiona kipaji cha mwanawe alianza kufunza mchezo wa tennis na kumuendeleza kucheza mchezo huo.

Kilichomfanya baba wa Osaka kutaka mwanawe awe mwana tennis ni kutokana na alivyokuwa akivutiwa na dada wawili kutoka nchini Marekani, Venus na Serena Williams walivyokuwa mabingwa wa mchezo huo.

Hata hivyo kulikuwa na ugumu kwa Leonard François kumfuza Osaka mchezo wa tennis hasa ikizingatiwa kuwa hakuwa ana upeo mkubwa sana kwenye mchezo huo ikilinganishwa na baba wa akina Venus na Serena aliyekuwa akiwafunza mwenyewe mchezo huo.

Kutokana na hali hiyo, alilazimika kutafuta miongozi na kujifunza hivyo baadae akaingia kiwanjani kuwafunza mabinti zake Naomi na Mari na mna ya kucheza mchezo huo na kuvikuza vipaji vyao.

Mnamo mwaka 2006 familia hiyo ilihamia katika mji wa Florida wakati huo Naomi akiwa na miaka tisa, ambapo baada ya kuwasili katika mji huo alipata fursa zaidi ya kutanua vipaji vya watoto wake katika viwanja vya wazi.

Alipotimiza umri wa miaka 15, Naomi alipelekwa katika chuo cha michezo ambapo alikuwa chini ya mkufunzi wa michezo aliyejulikana kwa jina la Patrick Tauma na mnamo mwaka 2014, alijiunga na chuo chengine kilichokuwa chini ya Harold Solomon Tennis Academy.

Pamoja na Naomi kukulia nchini Marekani wazee wake wamependelea binti yao awakilishe taifa la Japani kila atakapopata fursa za kuingia kwenye michuano ya kimataifa.

Katika taarifa ya pamoja ya wazee wa Naomi walisisitiza kuwa binti yao huo atawakilisha taifa la Japani pamoja na sababu mbalimbali chama cha tennis nchini Marekani awali hakikuonesha kumsaidia.

Hata hivyo Naomi alipofikia umri wa miaka 16, chama cha mchezo wa tennis nchini Marekani kilimuita kwenda kwenye kambi na mazoezi ya timu ya taifa, lakini alikataa wito huo.

Mnamo mwaka 2014 alishiriki kwenye michuano ya Stanford Classic, ambapo alifanikiwa kuingia kwenye fainali na kupambana na aliyekuwa bingwa wa michuano ya wazi ya Marekani kwa wakati huo, Samantha Stosur.

Miaka miwili baadae alifikia fainali kwenye michuano ya wazi Pan Pacific na kuingia kwa mara ya kwanza kwenye orodha ya wacheza tennis 50 bora wanawake duniani.

Mnamo mwaka 2018, Naomi alifanikiwa kutinga fainali kwenye michuano ya wazi ya Indian Wells, kabla ya mwaka huo huo kushiriki kwenye michuano ya wazo ya Marekani na kucheza fainali na Serena Williams ambapo alimchapa na kuwa mwanamke wa kwanza kutoka nchini Japani kutwaa taji hilo kubwa.

Mnamo mwaka 2020, Naomi aliorodheshwa kama mwanatenisi maarufu raia wa Japan aliyewahi kuorodheshwa namba moja duniani na Shirikisho la Tenisi ya Wanawake Duniani (WTA).

Naomi Osaka ndiye mwanatenisi wa kwanza mzawa wa bara Asia kuwahi kushikilia nafasi ya kwanza duniani katika tenisi ya mchezaji mmoja kila upande.

Kufikia sasa, anajivunia kutia kibindoni mataji matano ya WTA Tour, aliijinyakulia mataji mawili ya kwanza ya Grand Slam kwa mchezaji mmoja kila upande kwa kutawala michezo ya US Open na Australian Open mnamo 2018 na 2019 mtawalia.

Kwa mujibu wa ripoti Naomi kwa sasa ndiye mwanamichezo wa kike anayevutia zaidi kibiashara duniani, isitoshe, ndiye mwanamichezo wa kike anayelipwa mshahara mnono zaidi duniani, akiwa anashikilia nafasi ya 29 kati ya wanamichezo wanaolipwa mshahara mkubwa zaidi duniani.

Mnamo mwezi Mei mwaka 2020, Jarida la Forbes lilifichua kwamba Osaka alipita utajiri wa miaka minne wa Serena wa kuwa mwanamichezo wa kike anayelipwa vyema zaidi duniani baada kujizolea jumla ya shilingi bilioni 4.3 bilioni, fedha hizo zilizidi zile alizopata Serena mnamo 2019 kwa takriban shilingi milioni 161.

Osaka amekuwa balozi wa mauzo wa kampuni ya vifaa ya masuala ya usimamizi nchini Japan, IMG, tangu 2016, Aidha kampuni ya vifaa vya michezo ya Yonex nchini Japan imekuwa ikimpa Osaka raketi za tenisi tangu 2008.

Hadi kufikia sasa, yeye hutumia raketi aina ya Yonex Ezone 98. Nyuzi za raketi hiyo ni za aina ya Polytour Pro 125 na Rexis 130. Osaka amekuwa pia balozi wa mauzo wa kampuni nyingine ya vifaa vya michezo ya Nike tangu 2019.

Hadi alipotia saini mkataba wa miaka mitano na Nike, alikuwa balozi wa mauzo wa kampuni ya Adidas iliyokuwa ikilipwa kima cha shilingi milioni 30 milioni kwa mwezi kwa kipindi cha miaka minne.

Osaka pia hujiingizia fedha za ziada kwa kuwa balozi wa mauzo wa kampuni ya magari ya Nissan na kampuni ya vifaa vya kielektroniki ya Citizen Watch.

Yeye pia ni balozi wa mauzo wa kampuni za vyakula ya Nissin Foods, kampuni ya vipodozi ya Shiseido, shirika la utangazaji la Wowow na kampuni ya safari za ndege ya Nippon Airways (ANA).

Katika jambo ambalo hatolisahau ni lile lililotokea mwezi Januari 2019, ambapo alilazimika kukabiliana na kadhia ya ubaguzi wa rangi.

Naomi alioneshwa akiwa na ngozi nyeupe katika kibonzo cha matangazo cha kampuni Nissin company, inayotengeneza tambi za noodles, kinyume na muonekano wake, jambo hilo lilizua gumzo, na baadae kampuni ikaomba msamaha kwa kitendo hicho.

Naomi anajichukulia kama raia wa Japan, lakini anakabiliwa ubaguzi kwa kiasi cha kutokukubalika hasa kutokana na kuwa na rangi nyeusi ambayo ni asili ya baba yake.

Naomi anajichukulia kama mtu mweusi kutokana na kubaguliwa na wajapan kiasi cha wale wanaojiona weupe kumtenga.

Jina la Osaka alipewa na mama yake ili aweze jificha akiwa Japan. Na yeye Naomi Osaka anakiri kuna wakati huko Japan walikuwa wanamshangaa ngozi yake kwa nini ana jina la kijapan wakati ni mweusi na Japani si nchi ya watu weusi.

Kuna wakati aliwahi kusema kuwa hata bibi yake alighadhibishwa na hatua ya ngozi ya mjukuu wake kuwa mweusi na kufikia hatua ya kuhoji kwanini mama yake Naomi alikuwa na uhusiano na mtu mweusi.

Kwa sasa Osaka amejiunga kwenye mitandao ya kupinga ubaguzi wa rangi akionesha kuunga mkono harakati za kupinga ubaguzi wa rangi unaojulikana kama ‘Black Lives Matter’.

Kwa kufahamu athari za ubaguzi wa rangi, Naomi amekuwa akiwapa heshima waathirika weusi wa ubaguzi wa rangi wakati mwengine akiwapatia barakoa ili kujikinga na maradhi ya corona.

Naomi aliwahi kunukuliwa akiwashukuru mababu zake waliowazaa wazee wake kwa kusema, “ningependa kuwashukuru mababu zangu kwasababu kila wakati, ninapokumbuka kuwa damu yao inapita katika mishapa yangu inanikumbusha kuwa siwezi kushindwa”.

Amekuwa akikerwa na suala la ubaguzi wa rangi na katika kila mechi kwenye mashindano ya wazi ya Marekani yaliyopita alivalia barakoa yenye jina la mhanga mweusi wa ghasia zinazodaiwa kufanywa na polisi au za ubaguzi wa rangi nchini Marekani.

Mmoja baadhi ya makocha kwa Sascha Bajin anamuelezea Naomi kama binti mpole asiyependa kuongea na mwenye haya nyingi, hata hivyo anasema ni binti mwenye kujielewa na kuelewa kile anachokifanya.

Naomi na Cordae

Taarifa zilizopo ni kwamba binti huyo wa kijapani kwa sasa anatoka kimapenzi na na mwanamuzi wa kufoka foka anayejulikana kwa jina la Cordae, ambaye hujitokeza mara chache kumpa sapoti mpenzi wake huo anaposhuka kiwanjani.