NA MWAJUMA JUMA
WAANDAAJI wa michuano ya ndondo wameshauriwa kutoa masharti ya kutowatumia wachezaji ambao wanashiriki ligi kuu na kanda wanapoanzaisha mashindano hayo.
Ushauri huo umetolewa na wadau wa soka visiwani hapa walipozungumza na mwandishi wa habari hizi katika viwanja mbali mbali vinavyofanyika michuano hiyo.
Walisema pamoja na kwamba wao wanapenda kuangalia ndondo, lakini, ifike pahala waandaaji hao kushirikisha vijana ili waonekane na waweze kupata klabu za kuchezea.
Walieleza kwamba maana halisi ya michuano hiyo ya ndondo kama ambavyo wenyewe wanasema ni kuibua vipaji, lakini, kwa kuwatumia wachezaji wanaoshiriki ligi kuu au kanda hapo hujaibua bali unaminya kuonekana vipaji vya vijana wanaochipukia.
“Mimi napenda kuangalia ndondo, lakini, wakati mwengine hupata mashaka kujiuliza ninapowaona wachezaji ambao nawaangalia katika ligi na ndio hao hao ninaowaona katika ndondo”, alisema, Ali Juma wa Mwera.
Alisema ili kuendana na lengo thabiti la kuanzisha mashindano hayo ni vyema mashindano yao wakaweka idadi maalumu ya wachezaji wanaoshiriki ligi madaraja ya juu ili na hao vijana wapate nafasi.
“Utakuta timu nzima inaundwa na wachezaji aidha Mafunzo, KMKM, JKU au klabu nyengine ambayo inashiriki ligi kuu na kwa pengine wachezaji wawili tu au mmoja ndio ni kijana, sasa hapa lile lengo haliwezi kufikiwa”, alisema, Haji Abdalla.
Hata hivyo walisema kuwa katika mashindano kama hayo hufika mawakala wa wachezaji na waalimu kutafuta wachezaji lakini wanapokuta wachezaji hao kwa hao inakuwa ni ngumu kuwachukuwa.
“Lakini kama kutakuwa na masharti maalumu ni dhahiri vijana wetu wengi watapata fursa ya kuonesha vipaji vyao na kupata kuendelezwa”, alisema Said Mohammed wa Miembeni.
Akizungumzia kuhusu hilo kocha wa Mafunzo, Said Kwimbi alisema yeye kwa uoni wake anahisi ni bora wachezaji ambao tayari wamekuwa wasishirikishwe bali wachukuwe wachezaji kutoka madaraja ya chini ili wawasaidie kuwatangaza.
Alisema kuwa wakiwatumia wachezaji hao wa madaraja ya chini watakuwa wakicheza kwa ari kubwa ili kutaka kuwazidi wale ambao wapo juu na yeye kuiga mfano wake lakini bila ya hivyo hawatowasaidia.