PRISCA ULOMI NA FARAJA MPINA, DODOMA

ALIYEKUWA Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Faustine Ndugulile amekabidhi Ofisi kwa Waziri  wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,  Dk. Ashatu Kijaji na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumpa fursa ya kuhudumu katika wizara hiyo.

Dk. Ndugulile alieleza hayo katika hafla iliyoshuhudiwa na Menejimenti ya wizara hiyona kumpongeza Dk. Kijaji kwa kuteuliwa na kuapishwa kuwa Waziri wa wizara hiyo na kumzungumzia kuwa ni kiongozi makini, mwenye uwezo mkubwa na anaamini atakuwa na mchango mkubwa katika sekta ya habari, mawasiliano na TEHAMA

Aidha, Dk. Ndugulile aliishukuru Menejimenti ya wizara hiyo kwa ushirikiano waliompatia katika kufanya kazi ya kuijenga wizara hiyo na hatimaye kuongezewa majukumu mengine huku akiyataja baadhi ya mafanikio hayo ni kutengeneza mpango mkakati wa wizara, mabadiliko ya sheria mbali mbali, kuimarisha utendaji wa taasisi na kukamilisha muundo wa wizara

“Naomba watendaji wenzangu, kuendeleza mazuri yaliyofanyika na kwa nguvu ileile na muendelee kutekeleza mazuri mengi zaidi kwa kushirikiana kwa karibu na Dk. Kijaji kwa kuwa naondoka nikiwa ameiacha katika mikono salama,” alieleza Dk. Ndugulile.

Naye Dk. Kijaji alimshukuru na kumpongeza Dk. Ndugulile kwa kuweka misingi imara katika wizara hiyo na kufahamika kwa majukumu inayotekeleza kwa kuhakikisha watendaji wa Wizara hiyo na taasisi zake wanashirikiana kwa karibu katika kuwahudumia wananchi

Alisema kuwa Rais Samia baada ya kuingia madarakani alimuamini Dk. Ndugulile kuendelea kuiongoza wizara hiyo hivyo anapokea wizara hiyo huku akiamini kuwa kulikuwa na mtu imara aliyetengeneza mazingira mazuri ya kuendelea kutoa huduma bora za habari, mawasiliano na TEHAMA kwa wananchi

Aidha, alimuomba Dk. Ndugulile kuendelea kushirikiana na watendaji wa wizara hiyo kwa kuwa ni miongoni mwa wadau wakubwa katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya nchi kupitia majukumu wa wizara hiyo ambayo ni mtambuka na wezeshi kwa Wizara na taasisi nyengine.

“Sisi wote ni Watanzania lengo letu ni kuijenga Tanzania hivyo uzalendo wetu, upendo wetu pasipo chuki na umoja wetu ndio kitakachofanikisha kutimiza malengo tuliyojiwekea,” alisema Dk. Kijaji