MIONGONI mwa hazina ambazo taifa lolote hujivunia, ni aina ya utamaduni wake.
Zanzibar kama yalivyo mataifa mengine, imebarikiwa kuwa na historia kubwa hasa kwenye suala zima la utamaduni, ambao umekuwa kielelezo halisi cha urithi kutoka kizazi kimoja hadi chengine.

Utamaduni umekuwa na faida kubwa kwa wananchi na jamii kwa ujumla, japo kuwa imekuwa vigumu kwa wengine kulitambua hili, kwa sababu wanapotekeleza utamaduni wao hufanya kwa kujifurahisha zaidi.

Moja ya faida kubwa ya utamaduni ni ile ya kiuchumi, ambapo lipo kundi la watalii wanaofunga safari kutoka nchini kwao na kuja visiwani hapa kujifunza, kuziona na kuzishuhudia mila, silka na utamaduni wetu.

Kwa bahati nzuri baadhi ya watalii hao hufikia hata kuiga utamaduni huo, kwa mafano mara ngapi tumewaona wazungu wakipaka piko, ambayo haina madhara kama michoro ya tattoo wanazojichora.Aidha wapo watalii wanaotoka katika nchi zao na kuja kuangalia tu majengo yetu hasa yaliyoko Mjimkongwe na kwenye hifadhi nyengine kwa sababu majengo hayo ni kielelezo cha utamaduni wetu.

Hata hivyo cha kusikitisha ni kwamba upande wa ngoma zetu za asili ambazo ni sehemu muhimu ya utamaduni wetu hivi sasa zimemeanza kupotea.Ngoma zetu za asili zilizokuwa zikichezwa,kupigwa na kuimbwa na wazee wetu katika mitaa na vijiji vyetu leo hii hazipo tena, huku vijana wanaochipukia wakionekana kujikita zaidi na nyimbo za kimagharibi.
Kila nyumba unayopita vijana wanaimba bongo fleva, staili ya muziki ambayo ni zao la aina za nyimbo kutoka nchi za magharibi.

Vyombo vyetu vya habari vimezisahau kabisa ngoma zetu za asili kama kinyakunyaku, mkugo, bomu, mdundiko, boso, maumbwa, gonga, mkurungu, kirumbizi, gombe sugu, ndarandara, vanga, msondo na hata mchezo wa ngíombe

Kwa uchache kabisa tumebakiwa na ngoma kama vile kibati na msewe tena kwa sababu serikali imekuwa ikihahamisha kwenye sherehe rasmi,hata beni nalo nobe hivi sasa limekuwa adimu.

Kwenye mziki wa taarabu huko hakuzungumziki, kwa sababu taarab inayopigwa hivi sasa na kuhamaisha kwenye vyombo vya habari ni ile tunayodiriki kusema imekosa heshima.

Taarab ya leo inapopigwa haina tofauti sana na mziki wa dansi kwa maana kwamba lazima kijasho kikutoke ukenda katika mziki huo, na kama inachezwa kwenye uwanja wa vumbi ukitoka ukumbini ukajitie maji la si hivyo usingizi huwezi kuupata.

Taarab ya asili tunayoizungumza ni ile ambayo kanzu ama gauni la mwenye kwenda kwenye muziki huo, likitiwa udi au mafuta mazuri harufu yake haiwezi kupotea hata pale unaporudi nyumbani.

Tukizungumzia yale yaliyomo kwenye mashairi tena hapo ndio huwezi kusema, kwa sababu umetumika usanii mkubwa wa kuisarifu fasihi, jambo ambalo ni tofauti kubwa na nyimbo za taarab ya kisasa.Tunazungumza kwa ajili ya kukumbushana na kuona jinsi gani tunavyoelekea siko kwa kupoteza vitu vyetu vya thamani ambavyo pengine vyengine hata hatujaviandika vizuri.

Ushauri wetu ni kwamba kumalizika kwa tamasha la Mzanzibari kwa mwaka huu, iwe dira ya kujipanga kwa mwakani kwa kuonyesha uhalisia wa yale ambayo leo tumeanza kuyapoteza.

Tamasha la mwakani lijikite zaidi kwenye ngoma wetu za asili, pengine hili litawafumbua macho vijana wetu ili waweze kutambua na kuweza kushikamana vyema utamaduni wetu.
Kwa ufupi kabisa tunaweza kusema kila mwana jamii ana wajibu wa kuulinda na kuutetea utamaduni wetu.