NA MUHSIN ALI, SCCM

OFISA kitengo cha huduma za jamii, Amosi Maziku, amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la omba omba katika maeneo ya miji, jambo ambalo linasababisha kuondosha taswira na haiba ya mji wa Zanzibar.

Akizungumza ofisini kwake Vuga, amesema ni jambo la kushangaza kuona wanawake pamoja na watoto wanakaa mitaani na wengine wanapita madukani kwa lengo la kuomba.

Amesema, mwanzoni omba omba wengi walikuwa wakitokea Tanzania bara, lakin kwa sasa wengi wao ni wazawa kutoka Zanzibar.‘Kuna kipindi tulitaka kuwapiga picha na kuwatoa kwenye vyombo vya habari, jambo ambalo lilipunguza kasi yao’ alisema.

Aidha, amesema, serikali inaendelea na jitihada katika kuwasaida wanawake, watoto pamoja na walemavu ili kuondokana na tatizo hilo.

Amesema, zipo Taasisi za  ustawi wa jamii, Wizara ya Wanawake na Watoto, Nyumba za Wazee Sebleni, ambazo zipo kwa ajili ya kutatua changamoto zao.

‘Vipo vitengo maalumu vinavowasaidia ikiwemo kutoa mikopo ambayo itawaezesha kujikwamua kiuchumi’ alisema.

Sambamba na hayo, ameziomba Taasisi binafsi pamoja na wenye uwezo kuunga mkono jitahada za serikali katika kupunguza vitendo vya omba omba vilivyokithiri.

Mkuu wa kitengo cha Dini Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Sheikh Khalid Mohamed Mrisho, amesema hata katika sheria za dini ya Kiislamu zimekemea tabia za kuomba kwani ni jambo ambalo linachukiza mbele ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake (S. A.W).

Amesema jukumu kubwa walilonalo Kamisheni hiyo, ni kukusanya Zakka pamoja na sadaka zinazotolewa na Waislamu, ili kuwanufaisha wanaostahiki.

‘Tumekuwa tukifanya hivi kwa miaka mingi, kwa watu ambao wameleta sadaka zao kwa ajili ya wanyonge’ alisema.Amesema kitengo chao kimekuwa kikitoa elimu kupitia vyombo vya habari, ili kuijenga jamii bora ilioshiba maadili mema na kuepukana na mambo maovu.