NA MWANDISHI WETU, OMKR

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman ametoa wito kwa shirikisho la watu wenye ulemavu Zanzibar, kuhamasisha na kuelimisha wananchi kuendeleza maridhiano ya serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo ni muhimu katika kusaidia kujenga amani ya nchi.

Othman ameyasema hayo jana ofisini kwake Migombani alipozungumza na Uongozi wa Shirikisho la Jumuiya za Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (SHIJUWAZA).

Alifahamisha kwamba hatua hiyo ni muhimu kwani itasaidia katika kujenga amani ya kweli, hasa ikizingatiwa kuwa bila ya kuwepo amani kunaweza kuchangia kuongezeka idadi ya watu wenye ulemavu.

Alisema ni muhimu ajenda ya kuhubiri suala hilo ikabebwa na kila mmoja ama taasisi miongoni mwa wanajamii na kila mmoja kujiona na muhusika wa kuhubiri serikali ya umoja wa kitaifa.

Makamu huyo aliitaka jamii kuachana na utamaduni wa kufanya mambo na matendo yanayoweza kusababisha ajali na kuongeza idadi ya walemavu.

“Utakuta mtu anaendesha gari, ama baiskeli huku anasikiliza simu kwa kuwa anataka kumridhisha mtu mwengine na kusahau kwamba jambo hilo ni hatari na linaweza kusababisha ulemavu na kuongeza idadi ya watu wenye ulemavu”, alisema Makamu wa Rais.

Aliwaeleza wanajumuiya hiyo kwamba serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na watu wenye ulemavu katika kusaidia kutatua changamoto mbali mbali zinazowakabili.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Watu wenye Ulemavu Zanzibar, Ali Omar Makame aliishauri serikali kufanya utafiti mahususi ili kuibua na kufahamu sababu za kuongezeka tatizo la ulemavu Zanzibar.

Alisema kwamba pia kuna haja ya kuwepo jimbo la watu wenye ulemavu ili kupata uwakilishi wa watu wenye ulemavu katika vyombo vya kutunga sheria badala ya utaratibu wa sasa kupitia kwenye vyama vya siasa.