NA MWANDISHI WETU, OMKR

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, amesema Zanzibar na Oman zinaweza kutumia historia na uhusiano wa damu uliopo wa muda ili kuibua fursa mpya zaidi za uwekezaji ili kusaidia kukuza uchumi na maendeleo ya jamii.

Othman alieleza hayo jana ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar, alipozungumza na balozi mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar, Said Salim Al Sinawi.

Makamu huyo alisema kwamba yapo maeneo mengi ambayo kimsingi, yanaweza kujadiliwa zaidi na baadae kujengewa ushirikiano unaoweza kusaidia manufaa kwa Zanzibar na Oman.

Alimueleza balozi huyo kwamba suala la mahakama ya kadhi, fursa za masomo na kubadilishana uzoefu ni miongoni mwa maeneo muhimu ambayo serikali hizo mbili zinaweza kujadiliana na kukubaliana kuongezwa ushirikiano kwa kuwa yana mchango mkubwa katika historia ya Oman na Zanzibar.

Alisema kwamba Oman ina zoefu mkubwa katika kusimamia mahakama za kadhi na ni waanzilishi wa mahakama hiyo hapa Zanzibar, hivyo kuna umuhimu wa kuongeza ushirikiano katika kusaidia mbinu za uendeshaji na usimamizi wa mahakama hizo hapa Zanzibar.

Alisema Oman ina mchango mkubwa katika uanzishwaji wa mahakama hizo sio tu kwa Zanzibar, lakini na nchi nyengine za Afrika Mashariki ikiwemo Kenya na Uganda.

Alimueleza balozi huyo kwamba hivi sasa Zanzibar inatekeleza sera yake ya uchumi wa buluu na imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji ambayo yanaweza kutumika kama fursa ya kuendeleza uwekezaji na kusaidia nchi kukuza uchumi.

Makamu alisema kuna haja ya kutumia mijadala rasmi na isiyo rasmi ili kujadili maeneo zaidi na fursa nyengine za ushirikiano kiuchumi na kimaendeleo kati ya Oman na Zanzibar na hatimaye kusaidia kuviachia vizazi urithi bora.

Naye Balozi Al Sinawi alimueleza, Makamu wa Kwanza wa Rais kwamba, Oman ipo tayari kuendeleza ushirikiano wa kihistoria uliopo katika sekta mbali mbali na kwamba inaichukulia Zanzibar kuwa ni nyumbani kutokana na udugu wa damu uliopo kwa muda mrefu.