MANILA, Philippines
BONDIA raia wa Ufilipino, Manny Pacquiao, amesema, kazi yake ya ngumi imefika tamati ingawa wakuu wa timu yake ya ‘promosheni’ wamesema, mazungumzo ya kustaafu kwake bado.

Bondia huyo mwenye umri wa miaka 42 alipoteza mbele ya Yordenis Ugas mwezi uliopita na wengi wakitabiri kwamba huo ndiyo mwisho wake na huenda ikawa pambano lake la mwisho.

Wiki iliyopita, bondia huyo alikuwa ametangaza nia yake ya kuwania urais wa Ufilipino mwaka ujao.

Bingwa huyo wa zamani wa uzito wa nane aliiambia Toni Talks kuwa amemaliza ngumi.
“Kazi yangu ya ndondi tayari imekwisha”, alisema, Pacquiao.
“Nimefanya kwa sababu nimekuwa kwenye ndondi kwa muda mrefu na familia yangu inasema kuwa inatosha”.

Lakini, mkuu wa promosheni wa Pacquiao, Sean Gibbons, alisema, mazungumzo yoyote ya kustaafu bado.”Seneta ni mgombea wa urais na bado hajafanya uamuzi wowote juu ya maisha yake ya ndondi”, Gibbons aliiambia ‘Yahoo Sports’.
“Katika wiki chache zijazo atafanya uamuzi wa mwisho ikiwa atakuwa na zaidi au atastaafu”.