NA MADINA ISSA
BENKI ya watu wa Zanzibar (PBZ) kwa kushirikiana na kampuni ya mawasiliano ya simu za mikononi Tigo, imezindua mashirikiano yatakayowezesha kufanya malipo ya elektroniki wa upatikanaji wa huduma za serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar unaojuliakana kwa jina la GEPG.
Makubaliano hayo, yamefikiwa baina ya Mkurugenzi Muendeshaji wa PBZ, Dk. Muhsin Salum Masoud na ofisa mkuu kutoka kampuni ya Tigo Tanzania, Angenica Pesha hafla ambayo ilifanyika katika ukumbi wa PBZ Mperani.
Akizungumza mara baada ya makubalinao hayo, mkurugenzi huyo alisema PBZ, na Tigo imekuja na mpango huo ambao ni muhimu kwa Zanzibar utakowezesha wananchi wa Zanzibar kufanya malipo kwa serikali kupitia tigo pesa.
“Hili ni jambo zuri na litawarahisishia sana kurahisisha kufanya miamala ya serikali katika taasisi mbalimbali jambo ambalo nawapongeza watendaji wa kampuni ya Tigo kuwaza jambo hili”, alisema mkurugenzi huyo.
Aidha alisema kuwa PBZ wamefurahishwa na kuwa washirika katika suala hilo, na watajitahidi kuona huduma hizo zinakuwa nzuri kwa wateja wao na kuwa endelevu.
Sambamba na hayo, alisema kuwa huduma hizo zitakuwa kutoka nje ya nchi pia ataweza kutumia huduma hizo kwa urahisi na kusema kuwa jambo hilo, linakwenda sambamba na mkakati wao wa Benki kwa miaka michache inayokuja kuwa na benki ya kielektorinik.
Nae, ofisa mkuu wa Tigo Pesa Tanzania, Angenica Pesha alisema mfumo huo utawawezeshawateja wote wa Tigo waliokuwepo Zanzibar kufanya malipo ya bili zao kwa kutumia mfumo wa Kieletroniki kwa serikali unaojulikana kama GEPG.
Alisema ushirikiano huo umekuwa na lengo la kuwarahisishia wateja wao katika kufanya miamala kwa urahisi ambapo ni vyema waliona kuwa waungane na Benki ya PBZ.